Makala

MICHEZO NA AFYA: Ukosefu wa viwanja vya watoto kuchezea mijini ni kikwazo kwa ukuaji wao

January 21st, 2020 3 min read

Na SAMMY WAWERU

KILA anapopata muda wa ziada Rashid Saka huutumia kufanya mazoezi ya soka.

Mvulana Saka, 10, ni mwanasoka chipukizi, ambapo ni mdakaji hodari wa ngozi iliyoambwa na kushonwa.

Kocha wake Fredrick Ochieng anasifia kipaji hicho, “akipaliliwa ataibuka kuwa mojawapo wa makipa gwiji nchini na hata ulimwenguni”.

Hata hivyo, chipukizi huyo anayesomea katika shule ya msingi ya binafsi ya Golden Gate Academy, Nairobi, pamoja na mastaa wengine chipukizi wana tatizo moja tu, ukosefu wa uga bora wa kupalilia talanta zao.

Ni hali ambayo inazingira vipaji walioko maeneo ya mijini, hasa Kaunti ya Nairobi.

“Chini ya timu ninazonoa wanasoka; Githurai United na All Stars Githurai, miongoni mwa changamoto zinazotuhangaisha ni ukosefu wa uwanja,” adokeza kocha Fredrick.

Jiji la Nairobi na viunga vyake, uwekezaji wa nyumba na majumba ya kupangisha, umesheheni. Ni nadra kuona eneo au mtaa wenye uga.

Aghalabu, nyingi ya nyanja wanazochezea vijana na watoto, ni ploti zinazomilikiwa na watu binafsi na ambazo hazijajengwa. Kwa mfano, mtaa wa Zimmerman, Nairobi, hamna eneo maalum lililotengewa uga.

Kulingana na sheria za ujenzi, mtaa unapaswa kuwa na nafasi iliyotengewa eneo la watoto kuchezea.

Christopher Wanjau, mtaalamu binafsi wa masuala ya ujenzi, hasa ramani ya ujenzi, anasema kila mtaa unapaswa kuwa na uga.

“Kwa mujibu wa sheria za mamlaka ya kitaifa ya ujenzi, NCA, ukuaji wa mitaa unapoendelea sharti itengewe nafasi ya uwanja,” Wanjau asema.

Ni kigezo muhimu ambacho kimeonekana kupuuzwa na NCA pamoja na wawekezaji wa majengo ya kupangisha.

Sawa na ramani ya eneo kupaswa kuwa na barabara, mitaa inatakiwa kuwa na miundomsingi kama vile hospitali na shule za umma, ambazo zinapasa kuwa na uga wa watoto kunyoosha viungo vya mwili.

Isemwavyo, mtoto akilimbikiziwa masomo siku nzima bila kupata fursa ya kucheza, ukuaji wake hautakuwa kamilifu.

“Ratiba ya mtoto, inahitaji kuwa na saa au wakati wa kucheza kila siku, ili kusaidia viungo vyake kukua, sawa na mtoto mdogo anavyohitaji muda wa kulala bila usumbufu,” afafanua Esphan Wambui, muuguzi na mtaalamu wa masuala ya watoto.

Kulingana na Wambui, muda wa kucheza usiwe ule anaoratibiwa kuenda maeneo yenye zana za kama vile merry-go-round na boti za vidimbwi, ila aruhusiwe kuwa huru kwenye uwanja atangamane na watoto wenza, wacheze soka, riadha, basketiboli, raga, na michezo mingineyo.

“Akiwa na wenzake, bongo litapevuka, na atajifunza asiyojua, na namna ya kuishi na watu,” asisitiza.

Kila mwezi Zimmerman, baadhi ya raia wa Sudan, wanaoishi eneo hilo na mitaa jirani, hushiriki tamasha za nyimbo za jamii yao. Idadi huwa kubwa, lakini mahala pa kuendeshea shughuli hiyo ndipo kikwazo, na huishia kukutana katika mojawapo ya ardhi binafsi ambayo haijajengwa.

“Sisi hukongamana hapa kujaribu kuimarisha mila na tamaduni zetu kwa njia ya nyimbo, na kujuana zaidi,” mmoja wa raia hao akaambia Taifa Leo.

Nyimbo zao, zinazoimbwa kwa lugha yao, hujumuisha kuruka wakiwa wameshika mkwaju na usakataji ngoma.

Ni katika ardhi iyo hiyo ambayo kwa upeo wa macho ni ndogo, ambapo vijana huchezea soka, kuendesha baiskeli na michezo mingine. Ardhi hiyo pia ndiyo hutumika na wanafunzi wa shule mbalimbali eneo la Zimmerman “Mmiliki wa ardhi hii akianza ujenzi hatujui watakapokuwa wakichezea watoto wetu,” analalamika Irene Chepkoech, mwalimu na mzazi.

Sawa na Zimmerman, taswira yake inaenda sambamba na ya mtaa wa Githurai 44, ingawa mtaa huo una uga mmoja tu ulio pembezoni mwa shule ya msingi ya Githurai. Hali ya uwanja huo si ya kuridhisha, kwani umesheheni vumbi na ambayo ni hatari katika afya ya watumizi, hususan watoto.

“Huu ndio uga tulionao, umepuuzwa. Viongozi na wadau husika wanapaswa kuuimarisha, angaa kwa kupanda nyasi. Ni mahangaiko tele ninapopalilia vipaji vya wanasoka chipukizi,” ateta kocha Fredrick Ochieng.

Anasema juhudi zake kuwasilisha malalamishi kwa viongozi husika, umeonekana kukumbwa na siasa na pingamizi.

Mtaa wa Githurai 45, Progressive, Maguo, Mumbi na Mwihoko, matatizo ni yale yale, ya ukosefu wa eneo maalum vijana na watoto kuchezea. Majengo ya kupangisha pamoja na ya biashara yamesheheni.

Pembezoni mwa Thika Superhighway, kati ya mtaa wa Githurai 45 na Clayworks, kuna uga mmoja tu, wenye nyasi, ingawa ni ardhi binafsi.

“Eneo hili hakuna uga wa umma, kwa mfano wanafunzi wa Mwiki Primary, hufululiza hadi uwanjani huu ulio pembezoni mwa Thika Road,” mkazi Lawrence Kariuki akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano.

Ardhi hiyo, na inayosemekana kuwa na utata, wanafunzi wa Mwiki Primary hutembea takriban kilomita tano, kufanya mazoezi na kushiriki michezo. “Ni hatari wanafunzi kutembea masafa hayo ikizingatiwa kuna magari na pikipiki barabarani wanamopitia,” akasema Kariuki.

Taswira ya mitaa hiyo, si tofauti na ya mitaa mingine kama vile Mwiki, Kasarani, Roysambu, Lucky Summer, Kariobangi, na mingineyo Nairobi.

Uwanja wa Kimataifa wa Moi Sports Centre Kasarani (MISC), nao unaonekana kushirikisha klabu au timu tajika pekee.

Kulingana na Patrick Ogwayo, mtaalamu wa masuala ya soka, itachukua juhudi za serikali na wawekezaji kutathmini suala la kutenga ardhi maalum, katika kila mtaa mijini ili kujali masilahi ya watoto na vijana.

“NCA na asasi husika, kibarua ni kwao, la sivyo siku za usoni na kizazi kijacho hakitakuwa na mahala pa kuchezea,” asema.

Ogwayo anasema ardhi zinazotumika kama majaa, zinaweza kugeuzwa kuwa uga. Akitoa mfano wa mtaa wa Githurai 44, anasema mojawapo ya jaa ni hatari katika “kuchafua mazingira” na kwamba ardhi hiyo inaweza kuwa yenye manufaa ikiwa itatwaliwa na kutumika kama ukumbi wa kupalilia vipaji mbalimbali katika michezo, uwanja.