Michezo

Michezo ya Kecoso ilivyoacha kumbukumbu isiyofutika Kisii

August 22nd, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

MAKALA ya mwaka 2019 ya Michezo ya Mashirika ya Mawasiliano Nchini (Kecoso) yalidumisha dhamira yake ‘Kupeleka Michezo karibu na Wananchi’.

Mwenyekiti wa Kecoso, Bildad Kisero kwa pamoja na Serikali ya Kaunti ya Kisii pamoja na jamii nzima ya Abagusii wanastahili pongezi kwa jitihada zao zilizofanikisha maandalizi ya michezo hiyo.

Gavana wa Kisii, James Ongwae na kikosi chake kizima pia wanastahili pongezi kwa kuboresha uwanja wa michezo wa Gusii, ambao hutumiwa na Shabana FC, kwa mechi zake za nyumbani. Uwanja huo unaokaribia kufikia viwango vya kimataifa, ulivutia zaidi ya mashabiki 10,000 waliohudhuria michezo hiyo kila siku kuanzia Agosti 10 hadi Agosti 17.

Ulikuwa mwaka wa 40 kwa michezo hii kufanyika tangu ibuniwe mnamo 1978 kwa lengo la kuwaleta pamoja watu wa tabaka mbalimbali.

Mbali na kuwaleta pamoja wananchi, michezo ya mwaka huu iliimarisha uhusiano miongoni mwa Wakenya ambao walikuwa wametengana kufuatia fujo zilizotokea katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Hii ilikuwa mara ya pili michezo hiyo kufanyika katika Kaunti ya Kisii, baada ya eneo hilo kutunukiwa fursa hiyo kwa mara ya kwanza mnamo 1993.

Michezo ya mwaka huu ilishirikisha wanamichezo katika mashindano mbalimbali pamoja na riadha, vikapu, urushaji vishale, kandanda, netiboli, pool, tenisi, uogeleaji, snooker, voliboli na gofu.Wageni waliozuru Kisii walifurhia makaribisho ya hali ya juu kutoka kwa wenyeji, mbali na kuburudishwa na utamaduni wa Wakisii.

Michezo hiyo ambayo iliandaliwa kitaalamu na kufaulu kuliko ilivyofikiriwa, kadhalika iliwaleta pamoja wanamichezo kutoka mashirika mbalimbali na kuimarisha uwiano na utangamano.

Ufanisi wa michezo ya mwaka huu ulitegemea juhudi za mashirika wanachama, uongozi bora wa Baraza Kuu la Usimamizi, uungwaji mkono wa kamati andalizi, upeperushaji wa habari za michezo hiyo pamoja na kamati ya uuzaji. Makundi muhimu kama vile Minet Kenya yaliyojitolea kutoa huduma za bure za matibabu michezo hiyo ikiendelea kadhalika yaliwapa wakazi fursa ya kujua hali yao ya kiafya.

Wakati wa shughuli hiyo, zaidi ya mipira 3,000 ya kondomu ilitolewa kwa wakazi bila malipo, mbali na faida nyingine walizopata kwa kuwauzia wageni vyakula.

Biashara yanoga

Waendeshaji bodaboda, wamiliki wa kumbi za burudani pamoja na wenye hoteli katika kaunti hiyo vilevile walinufaika kwa kiasi kikubwa.

Michezo hiyo iliyoandaliwa katika uwanja wa Gusii pamoja na sehemu nyingine vikiwemo viwanja vya Kisii High School, kadhalika iligundua vipaji vipya.

Ni michezo ambayo iliwapa wananchi fursa ya kuonyesha vipaji vyao hadharani mbali na kuleta uhusiano mwema miongoni mwao.

Serikali ya Kaunti ya Kisii ikishirikiana na kamati simamizi ya Kecoso ilifanya kazi kubwa ambayo itazidi kukumbukwa milele kwa kuimarisha umoja miongoni mwa Wakenya waliofika huko kushiriki ama kushuhudia michezo hiyo.

Maafisa Wakuu wa mashirika mbalimbali akiwemo Ezekiel Mutua wa Bodi ya Kuainisha Filamu Nchini (KFCB), pamoja na Naim Bilal wa Shirika la Habari la KBC ni kati ya waliofuata timu zao, mbali na kushiriki katika mbio maalum.

Kwenye hotuba yake, Mutua ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Waandishi wa Habari (KUJ) alisema Kecoso ni zaidi ya michezo.

Waziri wa Michezo Amina Mohamed pia alihudhuria.