Michezo

Michezo yatengewa asilimia kubwa zaidi ya bajeti katika historia

June 11th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

SEKTA ya michezo imetengewa kiwango kikubwa zaidi cha fedha kwa mara ya kwanza katika historia kwenye bajeti ya kitaifa ya mwaka wa kifedha wa 2020-21.

Sekta hiyo ilipata nyongeza ya hadi asilimia 154 ya bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2019-20.

Hii ni baada ya Waziri wa Fedha, Ukur Yatani kutangaza kwamba Wizara ya Michezo imetengewa Sh14 bilioni.

Kiwango cha fedha zilizotengwa mwaka huu ni cha juu zaidi kuliko kile cha 2019-20 ambapo Wizara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni ilitengewa Sh5.3 bilioni pekee kutoka hazina ya kitaifa. Hii ni nyongeza ya Sh8.7 bilioni.

Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Nick Mwendwa amesema kiasi hicho cha fedha katika bajeti ya 2020-21 kitaimarisha kiwango cha makuzi ya michezo humu nchini.

Mwingine ambaye amefichua matumaini yake kwamba fedha hizo zitaboresha maendeleo ya sekta ya michezo baada ya mashirikisho kuwezeshwa ipasavyo, ni Oduor Gangla ambaye ni Rais wa Shirikisho la Raga la Kenya (KRU).

“Fedha hizi zitaimarisha hali ya uchumi miongoni mwa vijana wetu ambao watapata nafasi nyingi za kazi kupitia michezo ya kila sampuli. Kwa kushiriki michezo hiyo hadi viwango vya kitaifa, watakuwa pia wakiletea Kenya fedha za kigeni na kutoa majukwaa mwafaka zaidi kwa maendeleo ya sekta nyinginezo, husuna utalii na ujenzi,” akatanguliza Yatani.