Habari za Kitaifa

Michezo yazima milio ya risasi mpakani Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet

February 20th, 2024 2 min read

NA OSCAR KAKAI

AMANI imerejea katika maeneo hatari ya Kapushen na Kamologon mpakani mwa kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet huku kukikosekana kurekodiwa kisa chochote cha mashambulio kwa muda wa miezi mitatu sasa.

Milio ya risasi imetulia huku shughuli za kawaida zikirejea.

Haya yanatokana na kuwahusisha vijana na michezo.

Vijana wengi kutoka jamii hasimu ambao walikuwa wanahusika kwa ujangili na wizi wa mifugo, wamebadilika na kuanza maisha mapya kupitia kwa michezo katika eneo hilo.

Serikali ya kaunti kupitia kwa ofisi ya mwakilishi wa wadi ya Tapach Samuel Korinyang ilifadhili mashindano hayo.

Mnamo Jumamosi, kombe hilo lilivutia timu tisa.

Kales FC ikiibuka na ushindi na kupokea Sh20,000 baada ya kulilima Chebon FC mabao 2-1 katika uga wa Tangasia.

Mpango huo unalenga kutambua vipaji vya vijana ambavyo vilisahaulika wakati wa machafuko.

Injili hiyo mpya ya spoti imekuwa ikihusisha vijana ambao sasa wanaweza kutumia muda wao vyema.

Afisa mkuu wa michezo kwenye kaunti ya Pokot Magharibi Edwin Pkemei anasema kuwa kombe hilo halikuwa ni la kuleta burudani tu bali pia lilikuwa ni la kusaka vipaji vya wale ambao wataendelea hadi kwenye timu ya Taifa ya U-20.

Bw Pkemei alisema michezo ni chombo muhimu cha kuinua uchumi wa jamii.

Aliwahakikisha wanaoshiriki kuwa watatumia ndoto zao na kuwa wachezaji bora siku za usoni.

Naye Bw Korinyang alisema kuwa ni mara ya kwanza eneo hilo kutoripoti kisa chochote cha utovu wa usalama na kuwataka viongozi kutoka kaunti hizo mbili kuweka mipango ambayo itawaweka vijana kwenye shughuli na waweze kujipatia riziki kama njia mojawapo ya kukomesha ujangili.

Alisema kuwa shughuli za michezo zitawapa vijana mwangaza kuwa na nguvu pamoja na kuinua talanta za waliokuwa na kila aina ya maovu katika jamii.

Aliwataka wakazi kukumbatia amani akisema kuwa kuna haja ya kutumia michezo kwa kudumisha amani.

Alisema kuwa wanahusika kwa kusaka vipaji kama njia ya kubadilisha sura ya eneo hilo.

“Vijana wengi hawana kazi na wanakosa shughuli za kuwasaidia kupata njia halali za kuwafaa kupata riziki kwa njia halali,” alisema.

Alisema kuwa michezo huwapa vijana kutoka ukoo na makabila tofauti nafasi ya kucheza pamoja.

Waziri wa michezo katika Kaunti ya Pokot Magharibi Lucky Litole alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo itawahusisha wenyeji kwenye masuala ya kijamii kama hayo na kuhamasisha wakazi kuhusu athari za wizi wa mifugo na matumizi ya dawa za kulevia.

“Tunataka talanta zibuniwe na vijana wazitumie kupata fedha,” alisema Litole.

Mwezi Januari, Wizara ya Usalama wa Ndani iliajiri askari wa akiba (NPRs) kwenye maeneo ya mipaka ya kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet.

[email protected]