• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 8:50 AM
Aibu Kenya ikilimwa na Sudan Kusini nyumbani Kasarani

Aibu Kenya ikilimwa na Sudan Kusini nyumbani Kasarani

Na CECIL ODONGO

Mashabiki wa soka nchini jana waliondoka uwanjani Kasarani kwa ghadhabu na aibu baada ya timu ya taifa Harambee Stars kunyukwa 1-0 na Sudan Kusini kwenye mechi ya kirafiki.

Kenya walijipata nyuma kupitia bao la Tito Okello dakika ya pili kutokana na masihara ya beki Brian Mandela.
Okello anawajibikia Kenya Police ambayo inashiriki Ligi Kuu Nchini (KPL).

Sudan walishiriki mchuano huo siku chache tu baada ya kunyeshewa 5-0 na vigogo Mali kwenye mechi ya kufuzu Mataifa Bingwa Afrika (AFCON).

Wapenzi wa soka nchini walikuwa na ari na matumaini tele kuwa Kenya ingeibwaga Sudan Kusini siku chache tu baada ya kuipiku Qatar 2-1 ugenini Doha.

Ushindi dhidi Qatar, nambari 59 duniani na nchi iliyokuwa imeandaa mechi za Kombe la Dunia mwaka jana, ulishangiliwa kweli kweli nchini huku Kocha Engin Firat ambaye alikuwa adui wa wengi kutokana na matokeo mbovu, akigeuka ghafla na kusifiwa kama kocha ambaye atapeleka soka ya Kenya mbali.

Kenya ilipigiwa upatu kuipiku Sudan Kusini kwa kuwa inashikilia nambari 102 duniani huku taifa hilo linalokumbwa na vita vya mara kwa mara likiwa nambari 167 katika viwango vya Fifa.

Sudan inafundishwa na Kocha Stephen Hen na haifahamiki kama taifa la soka ila inajulikana kutokana na mzozo wa kivita na uongozi kati ya wanasiasa wake.

Mechi hiyo ilikuwa imehudhuriwa na mashabiki wengi hasa baada ya kuraiwa na video fupi ya Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.

Katika mechi ya jana, Firat alifanya badiliko moja tu ambapo Brian Mandela alichukua mahala pa Johnstone Omurwa.
Omurwa ambaye aling’aa dhidi ya Qatar alikuwa amerejea kwa klabu yake ya Estrela da Amadora ambayo iko Ligi Kuu ya Ureno. Klabu hiyo ina mechi ngumu wikendi hii dhidi ya mibabe FC Porto.

Kenya imekuwa ikitumia mechi hizo kujifua kwa mechi za kufuzu Kombe la Dunia mnamo 2026 ambapo imetiwa katika Kundi F. Timu nyingine katika kundi hilo ni Ushelisheli, Burundi, Gambia, Gabon na Côte d’Ivoire.
Mechi hizo zinaanza Novemba mwaka huu na Kenya itakuwa ikilenga kuandikisha historia kwa mara ya kwanza ili itinge Kombe la Dunia.

“Sijaridhishwa na jinsi ambavyo tumecheza.Tuliwaruhusu wapinzani wetu kumiliki mpira. Pia kipindi cha pili, tulikosa nafasi nyingi tena za wazi za kufunga,” akasema Kocha Engin Firat. “Tulikuja kama timu ambayo imedharauliwa ili tukaanza mchezo vizuri na kupata bao la mapema. Kushindwa na mali kulitufungua macho na tulikuwa tunarekebisha baadhi ya makosa ambayo yalitokea kwenye mechi hii,” akasema kocha wa Sudan Kusini.

  • Tags

You can share this post!

Simiu apasha misuli moto akimezea mate mamilioni ya Delhi...

Nasaka mwanamume ambaye atasubiri hadi ndoa ndio aonje tunda

T L