• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
Beldine ndiye kocha wa kike pekee KWPL

Beldine ndiye kocha wa kike pekee KWPL

NA TOTO AREGE

KOCHA wa timu ya Kenya Police Bullets FC Beldine Odemba, ndiye kocha mwanamke pekee ambaye ananoa timu ya wanawake katika Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL).

Kando na kunoa Bullets, ni kocha wa timu ya taifa ya Kenya ya wanawake ya Junior Starlets ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 18 na kocha wa timu ya soka ya wavulana wa Highway High School ya Nairobi.

Mwaka 2022, alioongoza Highway hadi fainali ya Michezo ya Shule za Afrika Mashariki (EASG) nchini Tanzania kwa mara ya kwanza kwenye historia.

Odemba pia alikuwa chini ya kocha Collins “Korea” Omondi katika timu ya Ligi Kuu ya Wanaume ya Shirikisho la Soka nchini (FKF-PL) Mathare United kama meneja.

Hili ni jambo la kupigiwa mfano ikilinganishwa kwamba, asilimia 99 ya timu za KWPL na timu za wanawake za taifa zinanolewa na makocha wa kiume.

Bullets awali iliitwa Thika Queens kabla ya kubadilisha jina iliponunuliwa na timu ya Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF-PL) Kenya Police FC miezi miwili iliyopita.

Kando na Odemba, msimu jana timu mbili pekee ziliongozwa na makocha wa kike. Kocha Benter Achieng’ aliongoza Thika Queens huku Mary Adhiambo akinoa makali ya Kayole Starlets.

Achieng’ aliongoza Thika kutwaa ubingwa wa ligi msimu wa 2022/21 KWPL.

Adhiambo kwa upande mwingine, alitwikwa majukumu ya kuiongoza Kayole wakati wa dirisha fupi  la uhamisho msimu jana.

Alichukua mikoba ya kocha Joshua Sakwa ambaye alipewa majukumu mengine kwenye klabu. Sakwa alikuwa mkufunzi tangia mwaka 2008.

Adhiambo ambaye aliwahi kuwa kocha msaidizi wa Harambee Starlets, alikuwa na kibarua kigumu cha kuiondoa Kayole kwenye hatari ya kushuka daraja na ambacho hakufanikiwa kukitimiza.

Kayole pamoja na Kisumu All Starlets na Kangemi Ladies walishuka daraja rasmi msimu jana.

Adhiambo aliongoza Starlets kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (AWCON) kwa mara ya kwanza mwaka 2016 akiwa kocha msaidizi.

  • Tags

You can share this post!

Haikuwa lazima kumtaja Obasanjo, Ichung’wah afokea...

Waitaliano wasitozwe ada ya Visa – mbunge

T L