• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
Bellingham atawazwa Mchezaji Bora wa Bundesliga 2022-23

Bellingham atawazwa Mchezaji Bora wa Bundesliga 2022-23

Na MASHIRIKA

KIUNGO wa Borussia Dortmund, Jude Bellingham ametawazwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) msimu huu.

Bellingham, 19, alikuwa mhimili muhimu kambini mwa waajiri wake muhula huu japo sare ya 2-2 dhidi ya Mainz katika siku ya mwisho ya kampeni ikashuhudia miamba Bayern Munich wakiwapokonya taji la Bundesliga kinywani.

Chipukizi huyo raia wa Uingereza alipachika wavuni mabao manane na kuchangia matano mengine katika mechi 31 alizosakatia Dortmund msimu huu.

“Majukumu yangu kikosini yamekuwa yakiongezeka kila mwaka. Lazima niendelee kujituma vilivyo na kuonekana katika kila idara uwanjani,” akatanguliza.

“Wachezaji wenzangu na wakufunzi wamechangia pakubwa kuimarika kwa kiwango cha mchezo wangu. Niliingia Dortmund nikijua mambo machache tu. Lakini sasa nimejifunza mengi katika ulingo wa soka baada ya usimamizi kunipa majukwaa mwafaka ya kudhihirisha uwezo wangu,” akaongezea.

Bellingham anahusishwa na uwezekano mkubwa wa kuingia katika sajili rasmi ya Real Madrid katika mpango utakaoshuhudia miamba hao wa Uhispania wakiweka mezani kima cha Sh14.8 bilioni.

Mwezi Aprili, Liverpool walijiondoa kwenye vita vya kufukuzia huduma za tineja huyo kwa sababu ya ukubwa wa gharama ya kumsajili. Hatua hiyo iliacha Real na Manchester City pekee katika kinyang’anyiro cha kupigania maarifa yake.

Bellingham alijiunga na Dortmund mnamo 2020 baada ya kuagana na Birmingham City kwa Sh4.2 bilioni. Tangu wakati huo, amechezea Dortmund zaidi ya mara 130 na kuwajibishwa na timu ya taifa ya Uingereza mara 24. Alikuwa miongoni mwa wanasoka waliotegemewa pakubwa na kocha Gareth Southgate alipoongoza Uingereza kutinga robo-fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Stephen Lenamarle achaguliwa Spika mpya wa Samburu

‘Nabii Yohana wa Tano’ aitwa afike mbele ya...

T L