• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 PM
Benki ya KCB yapiga jeki matayarisho ya Safari Rally kwa Sh150 milioni

Benki ya KCB yapiga jeki matayarisho ya Safari Rally kwa Sh150 milioni

NA GEOFFREY ANENE

KCB Bank Kenya itatumia Sh150 milioni kusaidia duru ya saba ya Mbio za Magari Duniani (WRC) Safari Rally itakayofanyika Juni 22-25 katika kaunti za Nairobi na Nakuru.

Benki hiyo itakayokuwa mshirika rasmi wa masuala ya kifedha ya WRC Safari Rally, imesema Sh100 milioni zitawekezwa moja kwa moja katika makala hayo ya 70.

Sh50 milioni zitapiga jeki madereva Evans Kavisi, Nikhil Sachania na bingwa wa Kenya 2022 Karan Patel pamoja na kutumiwa katika shughuli za kuvumisha bidhaa za KCB na kuimarisha uhusiano na wateja.

“Tangazo hili ni thibitisho la kujitolea kwa KCB katika kusaidia mashindano ya magari nchini. Tumetumia zaidi ya Sh1.5 bilioni kwa miaka 20 iliyopita, kilele kikiwa wakati Safari Rally katika ratiba ya dunia baada ya miongo miwili,” amesema Afisa Mkuu Mtendaji wa KCB, Paul Russo, akifichua kuwa benki hiyo imetumia Sh250 milioni katika Safari Rally tangu 2019.

Waziri wa Michezo Ababu Namwamba aliyehudhuria hafla ya kutangazwa kwa udhamini huo kwa Safari Rally na madereva watatu, amesema kuwa Kenya itaandaa mashindano makubwa kuimarisha sifa yake kama eneo la mashindano duniani.

KCB pia imetangaza kujitolea kwake katika kuendeleza shughuli za kulinda mazingira wakati wa michezo.Russo aliongeza kuwa KCB inashirikiana na washirika wengine katika mradi wa kupanda miti 400,000 katika kaunti kadhaa mwaka huu.

Kupitia ushirikiano huo, miti 700,000 ilipandwa mwaka 2022. Madereva waliothibitisha kushiriki mwaka 2023 ni pamoja na bingwa wa dunia na Safari Rally 2022 Kalle Rovanpera (Finland), Elfyn Evans (Wales), mshindi wa Safari Rally 2021 Sebastien Ogier kutoka Ufaransa, Mjapani Takamoto Katsuta, Wakenya Minesh Rathod, Karan Patel, Hamza Anwar, Jeremiah Wahome, Evans Kavisi na Nikhil Sachania na Martin Prokop (Czech) na Jasen Bailey (Canada).

Mwenyekiti wa Kamati Andalizi ya WRC Safari Rally, Carl Tundo, amesifu udhamini wa KCB akisema utasaidia sana katika kuhakikisha kuwa Kenya inaanda mashindano ya kufana.

Makala hayo yataanzia katika Bustani ya Uhuru jijini Nairobi, huku mikondo ikifanyika katika kituo cha kimataifa cha michezo cha Kasarani na eneobunge la Naivasha.

  • Tags

You can share this post!

Maajenti 60 wa Old Mutual watuzwa kwa kazi nzuri

Simbas yalenga kurarua Zimbabwe Currie Cup

T L