• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 5:55 AM
Bingwa Eliud Kipchoge asubiriwa na kibarua kigumu katika Berlin Marathon

Bingwa Eliud Kipchoge asubiriwa na kibarua kigumu katika Berlin Marathon

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA mara nne wa Berlin Marathon (2015, 2017, 2018 na 2022) Eliud Kipchoge anasubiri kwa hamu mtihani mkali katika makala ya mwaka huu yatakayofanyika nchini Ujerumani mnamo Septemba 24, 2023.

Runinga ya NTV ya Shirika la Habari la Nation (NMG) itapeperusha mbio hizo ambazo Kipchoge ni miongoni mwa washiriki 60,000.

Kwa ushirikiano na NMG, Ubalozi wa Ujerumani nchini Kenya pia umeandaa sehemu ya mashabiki kufuatilia mbio hizo kwenye runinga kubwa mjini Eldoret.

Kipchoge anashikilia rekodi ya Berlin Marathon ya wanaume na dunia ya mbio hizo za kilomita 42 ambayo ni saa 2:01:09 kutoka ushindi wake wa mwaka 2022.

Huenda akavizia tena rekodi yake ili kuiweka salama kwa sababu umri wake pia unasonga.

Kipchoge, ambaye atakuwa na umri wa miaka 39 hapo Novemba 5, alisikitisha katika nafasi ya sita katika Boston Marathon nchini Amerika mwezi Aprili kwa hivyo atakuwa akilenga kurejea ulingoni kwa kishindo.

Wapinzani wakuu wa bingwa huyo wa Olimpiki 2016 na 2021 ni pamoja na mfalme wa London Marathon 2022 Amos Kipruto kutoka Kenya (2:03.13), mshindi wa dunia mwaka 2015 Ghirmay Ghebreslassie kutoka Eritrea (2:05:34) na mshikilizi wa rekodi ya Ujerumani Amanal Petros (2:06:34).

Pia, kuna Wakenya Jonathan Maiyo (2:04.56), Eliud Kiptanui (2:05.21), Ronald Korir (2:05.37), Philemon Kiplimo (2:05.44), Enock Onchari (2:05.47), Mark Korir (2:05.49) na Josphat Boit (2:06:34), miongoni mwa washiriki kutoka mataifa mengine.

Macho yatakuwa kwa bingwa wa Berlin Half Marathon 2022 Sheila Chepkirui katika kitengo cha wanawake. Anajivunia muda bora wa 2:17:29. Anatarajiwa kuwa na kibarua kigumu dhidi ya Waethiopia 11 akiwemo Tigist Assefa (2:15:37). Mzawa wa Kenya Delvin Meringor, ambaye ni raia wa Romania, ana muda bora wa 2:20:49.

  • Tags

You can share this post!

Polisi waomba siku 14 kuwazuilia washukiwa 10 wanaohusishwa...

Haya machenza ya kwake yanasubiri kuchumwa tu!

T L