• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:55 PM
Bingwa wa riadha za wakongwe Sikuku atangaza kuvizia rekodi ya Afrika

Bingwa wa riadha za wakongwe Sikuku atangaza kuvizia rekodi ya Afrika

Na GEOFFREY ANENE

Bingwa wa mataji mawili ya dunia ya riadha za wakongwe za ukumbini Eric Sikuku ametangaza kuvizia rekodi ya Afrika ya kutembea haraka kilomita tano kwenye Riadha za Wakongwe za Afrika (AFMA) zitakazofanyika Novemba 16-18 ugani Pilditch mjini Pretoria, Afrika Kusini.

Sikuku anashiriki katika kitengo cha watembeaji walio chini ya umri wa miaka 45 (M45).

Anajivunia kukamilisha kilomita tano kwa muda wake bora wa dakika 22 na sekunde 15 alioandikisha wakati wa mashindano ya kuchagua timu ya taifa ugani Moi Kasarani mnamo Oktoba 27, ingawa haujaidhinishwa.

Sikuku ni mmoja wa wanariadha 10 watakaopeperusha bendera ya Kenya katika mashindano hayo yanayofanyika kila baada ya miaka miwili. Wakenya wengine ni Elizabeth Muthuka, Abednego Chesebe (200m/400m), Sylvia Chesebe (400m/800m), Geoffrey Kipkemboi (800m/1500m), Priscilla Biwott, Mercy Jepkemboi (5000m/nyika), Kenneth Mburu (10,000m/nyika), Rebecca Kerubo (kurusha tufe/weight/hammer throw) na Regina Mulatya (kuruka umbali/utatu).

Katika mahojiano na Taifa Leo mnamo Jumatano, Sikuku, 39, alifichua kuwa analenga kufuta rekodi ya Afrika ya matembezi ya haraka ya kilomita tano ya dakika 22:54.8 inayoshikiliwa na M. Whitmore.

“Nitakuwa Mkenya wa kwanza kujitosa ulingoni hapo Alhamisi na ninasubiri kwa hamu kubwa. Nina furaha kubwa kutimiza ndoto ya kushiriki mashindano haya. Nitajaribu kuvizia rekodi hiyo wala sio tu kutwaa taji,” alisema.

Sikuku ni bingwa wa dunia riadha za wakongwe matembezi ya haraka ya kilomita tano na pia 10km, mafanikio ambayo alipata mjini Malaga, Uhispania mwaka 2018.

Yeye pia ni bingwa wa Riadha za Dunia za Ukumbini za Wakongwe matembezi ya haraka ya mita 3,000m na 10km baada ya kutawala vitengo hivyo mjini Torun, Poland mwezi Aprili 2023.

Vilevile, Sikuku alishinda makala ya 13 ya Riadha za Afrika za Wakongwe matembezi ya 10,000m ugani Nyayo, Nairobi mwaka 2021.

Naibu meneja wa timu ya Kenya, Julius Kipkoech amesema kuwa timu hiyo imejiandaa vyema kwa siku tano zilizopita. “Tumekuwa na kambi ya mazoezi ya kufana ugani Nyayo. Tulifika hapa Pretoria vyema tayari kuendeleza ubabe wa Kenya katika mashindano haya. Tulikuwa wenyeji mwaka 2021 na kufanya vyema, kumaanisha kuwa tuna kibarua kigumu mbele yetu,” alisema Kipkoech.

  • Tags

You can share this post!

Seneta wa zamani katika kesi ya ulaghai wa gari adai...

Wakazi kuumia upya kaunti ikiongeza ada ya kuwakusanyia...

T L