• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Buffon aweka rekodi ya kuwa kipa mkongwe zaidi kuokoa penalti katika historia ya Serie A

Buffon aweka rekodi ya kuwa kipa mkongwe zaidi kuokoa penalti katika historia ya Serie A

Na MASHIRIKA

KIPA mzoefu Gianluigi Buffon, 43, aliokoa mkwaju wa penalti na kusaidia waajiri wake Juventus kuwapepeta Sassuolo 3-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) iliyoweka hai matumaini ya kikosi hicho kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao wa 2021-22.

Buffon ambaye ametangaza kwamba atabanduka kambini mwa Juventus mwishoni mwa msimu huu, alipangua penalti ya Domenico Berardi katika dakika ya 15.

Kiungo Adrien Rabiot aliwaweka Juventus kifua mbele katika dakika ya 28 kabla ya Cristiano Ronaldo kufunga bao lake la 100 akiwa mchezaji wa klabu hiyo kunako dakika ya 45.

Ingawa Giacomo Raspadori alipania kurejesha Sassuolo mchezoni kunako dakika ya 59, chombo cha kikosi hicho kilizamishwa kabisa na Paulo Dybala aliyefungia Juventus bao la tatu katika dakika ya 66.

Juventus ambao walikuwa wakijivunia rekodi ya kushinda taji la Serie A kwa kipindi cha misimu tisa mfululizo, walizidiwa ujanja msimu huu baada ya Inter Milan ya kocha Antonio Conte kutamatisha ukiritimba wao katika soka ya Italia.

Chini ya kocha Andrea Pirlo, Juventus kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la Serie A huku zikisalia mechi mbili zaidi kwa kampeni za muhula huu wa 2020-21 kutamatika rasmi.

Juventus wanahitajika sasa kupepeta Inter Milan mnamo Mei 15, 2021 na kusajili ushindi mwingine dhidi ya Bologna mnamo Mei 23 kwa matumaini kwamba Atalanta, AC Milan na Napoli watapoteza alama muhimu ndipo wao wakamilishe kampeni za Serie A msimu huu ndani ya orodha ya nne-bora ili kufuzu kwa kipute cha UEFA.

Hadi kufikia sasa, Buffon anajivunia kunyanyua jumla ya mataji 10 akiwa mchezaji wa Juventus katika awamu mbili tofauti. Mechi iliyowakutanisha na Sassuolo ilikuwa yake ya 657 katika Serie A japo ilikuwa yake ya saba pekee msimu huu.

Akiwa sasa na umri wa miaka 43 na siku 105, Buffon ndiye kipa mkongwe zaidi kuokoa penalti katika historia ya kipute cha Serie A.

Sasa ni pengo la alama moja pekee ndilo linatamalaki kati ya Juventus na nambari nne Napoli. Atalanta na AC Milan wanashikilia nafasi za tatu na nne mtawalia.

Mabao kutoka kwa Luis Muriel na Mario Pasalic yaliwapa Atalanta ushindi wa 2-0 dhidi ya limbukeni Benevento waliokamilisha mechi wakiwa na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya beki Luca Caldirola kuonyeshwa kadi mbili za manjano.

Ante Rebic alifunga mabao matatu na kusaidia AC Milan kupepeta Torino 7-0. Mabao mengine ya AC Milan ya kocha Stefano Pioli yalifumwa wavuni na Franck Kessie, Brahim Diaz na Theo Hernandez aliyefunga mawili.

Mabingwa wapya wa Serie A, Inter Milan walisajili ushindi wa 3-1 dhidi ya AS Roma uwanjani San Siro. Magoli ya miamba hao yalifungwa na Marcelo Brozovic, Matias Vecino na Romelu Lukaku. Roma watakaokuwa chini ya kocha Jose Mourinho kuanzia msimu ujao walifutiwa machozi na kiungo wa zamani wa Arsenal na Manchester United, Henrikh Mkhitaryan.

Zikisalia mechi mbili pekee kwa kampeni za Serie A msimu huu kukamilika rasmi, Atalanta wanashikilia nafasi ya pili jedwalini kwa alama 75 sawa na AC Milan. Napoli wanajivunia alama 73, moja kuliko Juventus.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kumbe maseneta ni wabwekaji wasio na uwezo kung’ata!

Sheffield United kumwajiri kocha Slavisa Jokanovic wa klabu...