NA TOTO AREGE
ZIKIWA zimesalia wiki mbili kabla ya msimu wa 2023/24 wa Ligi Kuu ya Wanawake nchini (FKF-WPL) kuanza rasmi, shughuli za klabu kununua wachezaji wapya zimeshika kasi.
Wageni katika FKF-WPL Bungoma Queens, wanaendelea kujipanga kabla ya msimu mpya kuanza.
Kando na Bungoma, timu ambazo pia zinatarajiwa kuleta ushindani ligini ni pamoja na Soccer Assasins, Madira Girls na Kibera Girls ambao pia walipanda daraja.
Bungoma ilianzishwa mwaka 2021 ikiwa katika ligi ya mkoa ambapo ilimaliza katika nafasi ya kwanza na moja kwa moja ikajiunga na Divisheni ya Kwanza mwaka uliofuata.
Katika msimu wa 2022/23 ambao ulikamilika Mei 2023, Bungoma walijikatia tikiti ya kujiunga na ligi kuu baada ya kuinyeshea Uweza Women 6-5 kupitia penalti. Mechi hiyo ilikuwa imekamilika kwa sare ya 1-1 kwenye muda wa kawaida.
Timu hiyo chini ya kocha Robert Majio na msaidizi wake Jairus Misiko, imeingia sokoni kusaka wachezaji wapya.
“Tayari wamefanya usajili wa wachezaji sita. Lengo letu msimu ujao ni kuibuka washindi wa ligi. Wachezaji wageni tayari wako kambini na wameanza kufanya mazoezi,” alisema Misiko.
“Kwa sasa tunatumia uwanja wa Chuo Anuwai cha Sang’alo katika Kaunti ya Bungoma. Msimu mpya tutatumia uwanja wa Sudi kama uwanja wetu wa nyumbani,” aliongezea Misiko.
Viungo Diminah Wayera, Ruth Nekeyo na Brenda Simiyu wamenaswa na Bungoma.
Wachezaji wengine ni pamoja na mshambulizi Ann Mukhebi, mabeki Linda Ruchu, Linda Oksai, Deborah Lavenda Waswa na Noel Oruko.
Walioondoka klabuni ni Martha Karani na Tumaini Waliaula ambao walijiunga na mabingwa watetezi Vihiga Queens.