• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 7:53 PM
Cameroon wawasili nchini kwa mechi ya marudiano dhidi ya Rising Starlets

Cameroon wawasili nchini kwa mechi ya marudiano dhidi ya Rising Starlets

NA TOTO AREGE

TIMU ya wanawake ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 ya Indomitable Lionesses ya Cameroon imetua jijini Nairobi kwa ajili ya mechi ya marudiano ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Rising Starlets ya Kenya.

Mechi hiyo itagaragazwa katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi mnamo Ijumaa kuanzia saa tisa jioni.

Kenya iliwasili nchini kutoka Cameroon mnamo Jumatatu baada ya kupokezwa kichapo cha 3-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza wa raundi ya tatu wikendi iliyopita.

Mechi hii ni muhimu kwa Kenya kwani, lazima ishindi kwa zaidi ya mabao manne bila kuruhusu hata bao moja ili kufuzu kwa raundi ya nne.

Mshindi, atakutana na mshindi kati ya Congo Brazzaville na Misri katika raundi ya nne na ya mwisho baadaye mwaka huu 2023.

Starlets chini ya kocha Beldine Odemba ilikumbana na changamoto kubwa kutokana na wachezaji wanane tegemeo kutokuwepo kikosini. Wachezaji hao hivi sasa wanaendelea kufanya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) unaoendelea kote nchini. Wanane hao walikuwa wachezaji muhimu katika kufuzu kwa raundi ya tatu, hasa kwa kuitoa Angola kwa jumla ya mabao 10-1.

Starlets wameendelea na mazoezi Jumanne katika uwanja wa Kasarani Annex jijini Nairobi.

Kulingana na nahodha wa timu hiyo, beki Rebecca Kwoba, hawakumakinika katika mechi dhidi ya Cameroon kutokana na mazingira kuwa mageni.

“Tulicheza kipindi cha kwanza tukiwa na presha na hili lilionekana. Katika kipindi cha pili hata ingawa hatukufunga, tulirejea sote motisha ikiwa juu na ndio maana hatukuruhusu bao. Tumekuwa na kikao chetu sisi wachezaji na tumekubali makosa yetu na kuhiari kujifunza kutokana na makosa hayo. Tunaendelea kujiimarisha mazoezini,” akasema beki Kwoba.

Naye winga Fasila Adhiambo amesisitiza kuwa lengo lao sasa ni kulipiza kisasi.

“Timu yetu ni bora kuliko Cameroon. Tuliadhibiwa kutokana na makosa machache ambayo hatukurekebisha mapema katika mechi hiyo. Tunawasubiri nyumbani na siku zote, mcheza kwao hutuzwa,” winga Adhiambo akatoa hakikisho.

Colombia itakiwa mwenyeji wa Kombe la Dunia, kuanzia Agosti 31, 2024, hadi Septemba 22, 2024.

Timu 24 zitawania kutwaa ubingwa.

  • Tags

You can share this post!

Washukiwa wa wizi wa Sh94m za Quickmart wazuiliwa kwa siku...

Mlalamishi mwingine aiomba korti kusitisha ada mpya za...

T L