NA TOTO AREGE
NDOTO ya timu ya taifa ya wanawake ya Rising Starlets ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 kufuzu kwa Kombe la Dunia U-20 imefifia, baada ya kupoteza 3-0 dhidi ya Indomitable Lionesses ya Cameroon ugenini Jumamosi.
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya tatu ilichezwa katika uwanja wa Stade Ahmadou Ahidjo nchini Cameroon.
Matokeo mabaya huko Cameroon yanamaanisha Kenya lazima izuie kufungwa zaidi ya mabao matatu au kushinda kwa tofauti ya mabao manne katika mechi ya marudiano itakayopigwa katika Uwanja wa Taifa wa Nyayo jijini Nairobi mnamo Ijumaa wiki ijayo.
Mechi hiyo itaamua timu itakayokabiliana na mshindi kati ya Congo Brazzaville na Misri katika raundi ya nne na ya mwisho baadaye mwaka huu 2023.
Mshambulizi Annie Engamembem alikuwa wa kwanza kucheka na wavu katika dakika ya 21 na kuongeza uongozi wao kwa bao jingine katika dakika ya 36 kutokana na makosa ya ulinzi.
Engamembem amefungia timu yake ya taifa mabao sita katika mechi tano tu.
Bao la Naomi Eto dakika ya 44 liliimarisha zaidi nafasi ya Cameroon kufuzu Kombe la Dunia.
Ingawa hivyo, Starlets walipata pigo kutokana na kutokuwepo kwa wachezaji wanane muhimu, ambao kwa sasa wanafanya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) unaoendelea kote nchini.
Wachezaji hawa walikuwa muhimu katika kufuzu kwa raundi ya tatu, hasa kwa kuondoa Angola kwa jumla ya mabao 10-1.
Kombe la Dunia litaandaliwa nchini Colombia kuanzia Agosti 31, 2024, hadi Septemba 22, 2024, na timu 24 zitapambana kwa tuzo kubwa kwenye jukwaa kubwa.
Itakuwa mara ya tatu kwa Colombia kuwa mwenyeji wa mashindano ya Fifa lakini mara ya kwanza kuwa mwenyeji wa mashindano ya wanawake.