• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 7:22 PM
CECAFA: Vihiga Queens kuvaana na Buja Queens kusaka nafasi ya tatu

CECAFA: Vihiga Queens kuvaana na Buja Queens kusaka nafasi ya tatu

NA TOTO AREGE

VIHIGA Queens wanapania kuaga dimba la Mashirikisho ya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa kishindo watakapomenyana na Buja Queens ya Burundi katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu.

Mechi hiyo itagaragazwa ugani Fufa Technical Center mjini Njeru, Uganda mnamo Jumatano.

Vihiga ambao ni mabingwa wa CECAFA 2021, walishindwa kufuzu kwa fainali Jumapili, baada ya kulazwa 2-1 na CBE ya Ethiopia. Mechi iliisha 1-1 katika muda wa kawaida.

Kwa upande mwingine, Buja waliadhibiwa 3-1 na ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Queens ya Tanzania katika nusu fainali katika uwanja uo huo.

Akizungumza wakati wa mahojiano ya kabla ya mechi siku ya Jumanne huko Njeru, kocha wa muda wa Vihiga Charles Okere alisema bado ana matumaini na kikosi chake.

“Tulikuwa na mchezo mgumu sana dhidi ya CBE tukiwa tumecheza dakika zote 120. Wachezaji wangu hawakumakinika katika dakika za mwisho za mchezo ndiposa tukaadhibiwa,” alisema Okere.

Kati ya wachezaji 11 wa Buja walioanza dhidi ya JKT kwenye nusu fainali, Wakenya sita akiwemo Corazone Aquino (kiungo), Elizabeth Wambui (winga), Topister Situma (mshambuliaji), Monicah Karambu (kipa), Lydia Akoth (kiungo), Ruth Ingotsi (beki) na Rachael Muema (kiungo) walikuwa kikosini.

Kiungo mwingine wa Kenya, Dianah Wacera, pia yuko kwenye kikosi cha Buja.

“Ni kama tutakuwa tukikabiliana na timu ya pili ya Kenya ambao nusu ya timu ina Wakenya. Tutapambana nao,” aliongeza Okere.

Wachezaji hao wa Harambee Starlets walijiunga na Burundi kwa mkataba wa miezi miwili.

Kocha wa Buja Feruzi Haruna alikuwa ameeleza hapo awali kwamba, kuongezwa kwa Wakenya kwenye timu kuliwasaidia kuziba mapengo mengi.

Katika fainali ya mwisho ya siku, CBE watamenyana na JKT kwenye uwanja uo huo.

Mshindi kati ya CBE na JKT, atawakilisha kanda la CECAFA katika mashindano ya Vilabu Bingwa Afrika (CAF) nchini Cote d’Ivoire mwezi Novemba 2023.

  • Tags

You can share this post!

USHOGA: Sheria tata yaanza kazi mshukiwa wa kwanza...

Polisi wasubiri mshtakiwa ajisaidie wapate pete

T L