• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 2:56 PM
Chepng’etich aweka rekodi mpya ya Kenya ya mita 1,500 Rome Diamond League, Conseslus ala hu!

Chepng’etich aweka rekodi mpya ya Kenya ya mita 1,500 Rome Diamond League, Conseslus ala hu!

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Faith Chepng’etich aliweka rekodi ya kitaifa ya mbio za mita 1,500 baada ya kumaliza nyuma ya Mholanzi Sifan Hassan mjini Rome, Italia, Juni 10.

Bingwa wa Olimpiki, Jumuiya ya Madola na Dunia Chepng’etich alitimka mizunguko hiyo mitatu kwa dakika 3:53.91. Alivunja rekodi yake ya kitaifa ya dakika 3:56.41 aliyotimka mjini Eugene nchini Amerika mnamo Mei 28 mwaka 2016.

Sifan, ambaye alikuwa ameshinda mbio za mita 10,000 kwa rekodi ya dunia ya dakika 29:06.82 mjini Hengelo nchini Uholanzi mnamo Juni 6, alitwaa taji la Rome la mita 1,500 kwa dakika 3:53.63. Muda wake ni rekodi ya duru ya Diamond League ya Rome na pia bora katika mizunguko hiyo mitatu mwaka 2021.

Muingereza Laura Miur alikamilisha nafasi tatu za kwanza kwa dakika 3:55.59. Muethiopia Letesenbet Gidey aliimarisha rekodi ya dunia ya Sifan ya mita 10,000 hadi 29:01.03 mnamo Juni 9 mjini Hengelo.Hapo Alhamisi, Conseslus Kipruto alishindwa kumaliza mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji ambazo Mmoroko Soufiane El Bakkali alitawala kwa dakika 8:08.54.

Muethiopia Bikila Takele (8:10.56) na Mohamed Tindouft kutoka Morocco (8:11.65) waliridhika katika nafasi ya pili na tatu, mtawalia. Wilberforce Kones kutoka Kenya pia aliishiwa na pumzi kabla ya kukamilisha mbio hizo za kuruka viunzi mara 28 na maji mara saba.

Mkenya wa kwanza katika mbio za wanaume za mita 5,000, Robert Koech aliandikisha muda wake bora akikamilisha katika nafasi ya nane kwa dakika 13:12.56. Nafasi tatu za kwanza zilinyakuliwa na Jakob Ingebrigtsen kutoka Norway (12:48.45), Muethiopia Hagos Gebrhiwet (12:49.02) na Mohammed Ahmed kutoka Canada (12:50.12).

Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya 12:35.36, Joshua Cheptegei kutoka Uganda alikamata nafasi ya sita (12:54.69). Dur ijayo ya Diamond League ni Julai 1 mjini Oslo, Norway.

  • Tags

You can share this post!

FKF yafanikisha klabu 11 za Nairobi kupokea chanjo ya pili...

Kalonzo, Raila kufufua NASA