• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Chipu wakamilisha kambi ya mazoezi ya Kombe la Afrika

Chipu wakamilisha kambi ya mazoezi ya Kombe la Afrika

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Kenya ya raga ya wanaume ya wachezaji 15 kila upande ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 maarufu kama Chipu, ilikamilisha kambi yake ya tatu ya mazoezi Jumatatu.

Chipu, ambayo inatiwa makali na kocha Curtis Olago, inajiandaa kutetea taji lake la Kombe la Afrika maarufu kama Barthes Trophy mnamo Juni 26 hadi Julai 3 ugani Nyayo mjini Nairobi.

Olago aliambia Taifa Leo mnamo Jumanne kuwa maandalizi yamekuwa mazuri. Hata hivyo, alikiri pia kuwa janga la virusi vya corona liliathiri pakubwa matayarisho.

“Tumekuwa mazoezini kwa majuma matatu. Tumekuwa na kambi ya mazoezi mara mbili mjini Nakuru na moja hapa Nairobi. Kwa sasa, hali kambini iko sawa,” aliongeza kocha huyo mkuu wa klabu ya KCB inayoshiriki Ligi Kuu ya wanaume (Kenya Cup).

Olago ana wachezaji 36 kambini. “Sitapunguza kikosi hiki, ingawa kila siku ya mechi nitakuwa nikitumia wachezaji 23.”Katika Barthes Trophy 2021, Chipu watavaana na Senegal (Juni 26), Madagascar (Juni 29) na Namibia (Julai 3).

Hata hivyo, vyombo vya habari nchini Namibia vimedai kuwa Namibia imejiondoa kutokana na marufuku ya serikali nchini humo dhidi ya michezo ya kugusana inayolenga kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.“Shirikisho la Raga nchini Namibia (NRU) linasikitika kujulisha Shirikisho la Raga Afrika kuwa limeondoa timu ya Under-20 katika mashindano ya Barthes Trophy kutokana na hali iliyoko sasa.

Hatuwezi kufanya mazoezi na kujiandaa vizuri kwa mashindano hayo,” gazeti la The Namibian lilinukuu rais wa NRU Corrie Mensah akisema. Marufuku dhidi ya michezo ya kugongana nchini Namibia imeratibiwa kutamatika Juni 30. Mshindi wa Barthes Trophy hufuzu kuwakilisha Afrika katika Kombe la Dunia la daraja ya pili (JWRT).

You can share this post!

Kevin de Bruyne ajumuika na wenzake kambini mwa Ubelgiji...

Phil Foden wa Man-City ndiye mwanasoka mwenye thamani ya...