• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Dereva Takamoto Katsuta alenga kumakinika kwenye mbio za Safari Rally

Dereva Takamoto Katsuta alenga kumakinika kwenye mbio za Safari Rally

Na GEOFFREY ANENE

MJAPANI Takamoto Katsuta anatumai kuandikisha matokeo mazuri kwenye raundi ya saba ya Mbio za Magari Duniani (WRC) Safari Rally katika kaunti za Nairobi na Nakuru mnamo Juni 22-25.

Dereva huyo kutoka timu ya Toyota Gazoo Racing (GR Yaris R1) amekuwa na mwaka 2023 mbaya.

Katsuta anayeelekezwa na Aaron Johnston anakamata nafasi ya nane kwa alama 23 baada ya duru za Monaco, Uswidi, Mexico, Croatia, Ureno na Italia.

Yuko nyuma ya Kalle Rovanpera kutoka Finland wa Toyota (pointi 118), Mbelgiji Thierry Neuville wa Hyundai (93), Ott Tanak kutoka Estonia wa M-Sport (85), Muingereza Elfyn Evans wa Toyota (83), Mfaransa Sebastien Ogier wa Toyota (70), raia wa Finland Esapekka Lappi wa M-Sport (67) na Mhispania Dani Sordo wa Hyundai (36).

Takamoto alikamata nafasi ya tatu katika Safari Rally 2022 baada ya kumaliza nyuma ya Rovanpera na Evans walionyakua nafasi mbili za kwanza katika eneobunge la Naivasha, mtawalia.

Mjapani huyo alikuwa nambari mbili nyuma ya Ogier katika Safari Rally 2021 wakati mashindano hayo yalifanyika kwa mara ya kwanza kwenye ratiba ya WRC tangu 2002.

“Hatujakuwa na msimu mzuri kufikia sasa, lakini tutajinyanyua katika duru ya Afrika! Umekuwa msimu mgumu, lakini sasa Safari Rally yaja nchini Kenya! Kutoka sasa ni wakati wa kupata matokeo mazuri,” aliapa.

Makala ya Safari Rally 2023 yamevutia zaidi ya madereva 30 wakiwemo bingwa wa dunia Rovanpera, mshindi wa Afrika kitengo cha chipukizi Hamza Anwar na bingwa wa Kenya, Karan Patel.

  • Tags

You can share this post!

Nakhumicha azitaka hospitali zisiwafukuze wagonjwa...

Fainali ya Klabu Bingwa Ulaya: Guardiola asipobeba taji...

T L