NA MWANGI MUIRURI
SENETA maalum Karen Nyamu ameweka kando mada ya mapenzi na sasa anaangazia gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) akisema matamanio yake ni kuona Manchester United ikijikwaa katika msimu wa 2023/2024.
Amesema kwamba katika kila mchuano ambapo Man U itakuwa ikivaana na timu pinzani, atakuwa akitamanani vijana wa Erik Ten Hag waangushwe.
“Katika michuano yote ya Man U katika EPL, mimi nitakuwa mpinzani wao kwa mara zote hizo,” akasema kupitia chapisho kwenye ukurasa wa Facebook.
Alisema kwamba raha yake ni Man U washushwe daraja ikiwezekana.
“Mimi kama mfuasi sugu wa Arsenal naapa ya kwamba nitakuwa muaminifu kwa wapinzani wa Man United kwa siku zote zile… Matumaini yangu yakiwa hii timu itakuwa na msimu wa kusikitisha,” akasema.
Katika msimu wa 2022/23, Arsenal ilimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Manchester City huku Man U wakimaliza katika nafasi ya tatu.