• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Everton yapepeta Southampton na kuweka hai matumaini ya kuingia 4-bora EPL

Everton yapepeta Southampton na kuweka hai matumaini ya kuingia 4-bora EPL

Na MASHIRIKA

MKUFUNZI Carlo Ancelotti amewataka Everton kujituma vilivyo na kuingia ndani ya mduara wa nne-bora katika jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Hii ni baada ya ushindi wa 1-0 waliousajili dhidi ya Southampton mnamo Jumatatu usiku kuwapaisha hadi nafasi ya saba kwa alama 43 sawa na mabingwa watetezi wa EPL, Liverpool.

Ni pengo la alama mbili pekee ndilo kwa sasa linatamalaki kati ya Everton na nambari nne West Ham United ya kocha wa zamani wa Manchester United, David Moyes.

Nafuu zaidi kwa Everton ni kwamba wana mechi moja zaidi ya kutandaza ili kufikia idadi ya michuano ambayo imesakatwa na washindani wao wakuu ligini, wakiwemo Liverpool, Chelsea, West Ham na nambari tatu Leicester City.

Man-United wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 50, sita kuliko Chelsea wanaokamata nambari tano. Manchester City wanaojivunia alama 62 kileleni mwa jedwali ndio wanaopigiwa upatu wa kutwaa ufalme wa EPL muhula huu chini ya kocha Pe Guardiola ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Barcelona na Bayern Munich.

Wakicheza dhidi ya Southampton mnamo Machi 1, Everton walifungiwa bao la pekee na la ushindi kupitia kwa Richarlson Andrade katika dakika ya tisa baada ya fowadi huyo raia wa Brazil kumzidi ujanja kipa Fraser Forster.

Kikosi hicho kitaruka Liverpool na Chelsea na kuingia ndani ya nne-bora jedwalini iwapo kitazamisha chombo cha West Bromwich Albion kwenye gozi litakalowakutanisha uwanjani The Hawthorns mnamo Machi 4, 2021.

Ushindi dhidi ya Southampton mnamo Jumatatu usiku ulikuwa wa kwanza kwa kikosi cha Everton kusajili katika uwanja wao wa Goodison Park tangu Disemba 19, 2020.

Everton wangalifunga mabao zaidi katika kipindi cha kwanza ila kipa Fraser akajitahidi kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na Richarlison, Gylfi Sigurdsson, Michael Keane na Dominic Calvert-Lewin.

Kichapo ambacho The Saints walipokezwa kilikuwa cha nane kutokana na mechi tisa na kwa sasa wanashikilia nafasi ya 14 kwa alama 30. Ni pointi saba pekee ndizo zinatenganisha Southampton ya kocha Ralph Hassenhutl na Fulham ambao kwa pamoja na West Brom na Sheffield United, wako katika hatari ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa msimu huu.

Southampton waliojitosa ugani kwa minajili ya mechi hiyo baada ya kupigwa 3-0 na Leeds United, sasa wanajiandaa kupepetana na Sheffield United mnamo Machi 6, 2020 ugani St Mary’s.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Hali tete Barcelona raia wa zamani na watatu wengine...

Twitter kuwazima milele wanaopotosha kuhusu chanjo ya corona