• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 6:02 PM
Firat motoni kwa kupuuza wachezaji wa Gor, Tusker na Ingwe kikosini Harambee Stars

Firat motoni kwa kupuuza wachezaji wa Gor, Tusker na Ingwe kikosini Harambee Stars

NA CECIL ODONGO

KOCHA wa Harambee Stars Engin Firat amekashifiwa vikali kwa kuwaacha nje wachezaji wa Gor Mahia, AFC Leopards na Tusker kwenye kikosi alichochagua kwa mechi za kirafiki dhidi ya Qatar na Sudan Kusini mwezi ujao.

Jana, Firat aliteua wachezaji 24 ambao wataingia kambini kuanzia Jumapili kwa ajili ya mechi hizo mbili.

Kenya itacheza na Qatar, wenyeji wa Kombe la Dunia 2022, ugenini mnamo Septemba 7 kisha dhidi ya Sudan Kusini mnamo Septemba 12.

Hakuna mchezaji kutoka mabingwa wa Ligi Kuu (KPL) Gor Mahia, Tusker walioibuka nambari mbili na hata AFC Leopards ambayo imesajili wanasoka wazuri, ambaye anaunga kikosi kilichotajwa jana.

Kenya Police ndiyo timu ambayo ilipata wachezaji wengi katika kikosi hicho baada ya mnyakaji Patrick Matasi, kiungo Kenneth Mugana, mvamizi Elvis Rupia na mabeki David ‘Cheche’ Ochieng na Aboud Omar kuteuliwa.

Wengi wa wachezaji waliopewa nafasi na Firat hucheza nje ya nchi.

Kwa mujibu wa mkuu wa Muungano wa Makocha Nchini Bob Oyugi, kikosi kilichoteuliwa kinadhihirisha ubaguzi nchini na kuzua maswali kuhusu utaalamu wa Firat kama kocha.

“Tangu apokezwe wadhifa huu, Firat hajaonekana ana mikakati yoyote ya kufufua soka ya Kenya. Amewahi kunukuliwa mara kadhaa akisema anajenga kikosi cha soka cha baadaye ila mambo yanaenda kinyume,” akasema Oyugi.

Jagina wa Gor Mahia Maurice ‘Sonyi’ Ochieng’ naye alisema kuwa hata enzi zake hakuna wakati mchezaji kutoka Tusker, Gor au AFC alikosekana Harambee Stars.

“Lazima kuwe na tatizo kwenye uteuzi huo kwa sababu huwezi kuwa na kikosi bila hata mchezaji mmoja kutoka Gor na AFC,” alitanguliza.

Huwa nafuatilia soka na hata baadhi ya wachezaji wa kigeni ambao wamejumuishwa katika kikosi hicho hawastahili kabisa,” akasema Sonyi, 75 kutoka nyumbani kwake Wang’arot, Kaunti Ndogo ya Seme.

Baadhi ya Makocha ambao hawakutaka wanukuliwe pia walizua maswali kuhusu kikosi kilichoteuliwa jana huku wakihoji kuwa baadhi ya wachezaji bora waliachwa nje.

Mechi hizi za kirafiki zinakuja baada ya Harambee Stars kushiriki nyingine ambazo zilihusisha timu nne mnamo Juni kule Mauritius.

Kenya ilishinda Pakistan 1-0 ila ikachapwa kwa idadi sawa ya mabao na Mauritius katika mashindano hayo.

  • Tags

You can share this post!

Naibu Spika ataka polisi sasa waanze kuvalia kamera mwilini...

Baba azuiliwa kwa siku 14 uchunguzi wa mauaji ya mwanawe...

T L