• Nairobi
  • Last Updated June 2nd, 2023 8:58 PM
Gaspo Women kususia mechi dhidi ya Vihiga Queens

Gaspo Women kususia mechi dhidi ya Vihiga Queens

NA AREGE RUTH 

GASPO Women huenda wakapata adhabu kali, ikiwa hawatacheza mechi yao ya mwisho wa msimu wa Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) Jumamosi, dhidi ya mabingwa Vihiga Queens katika uwanja wa GEMS Cambridge.

Gaspo kupitia mitandao yao ya kijamii Jumanne jioni walisema, hawatacheza dhidi ya Vihiga “kutokana na sababu za ndani.”

Mwenyekiti wa klabu ya Gaspo Edward Githua ameambia Taifa Spoti kwamba uamuzi waliofanya ulikuwa wa mwisho baada ya kufanya mashauriano na maafisa wakuu serikalini.

“Wachezaji walifikia makubaliano kwamba hawatapatikana kwa uteuzi na hatutawalazimisha. Huo ni uamuzi wao na tunauheshimu,” alisema Githua.

“Tayari tumeandikia Shirikisho la Soka nchini (FKF) barua. Wawape kombe Vihiga Queens hata kama hatupo… hatuna shida na hilo,” aliongezea Githua.

Kifungu cha 3.1.7 cha sheria na kanuni za FKF kinabainisha kwamba: “Klabu itakayoshindwa kuhudhuria mechi yoyote ya ligi/mashindano itawasilisha maelezo kwa maandishi kwa Kamati ya Ligi ya Kitaifa na Mashindano ya FKF ndani ya saa 48 kuanzia tarehe ya mechi.”

Kifungu 3.1.10. cha katiba kinaelezea zaidi kuwa: “Ikiwa maelezo kama ya 3.1.7 hayatakubaliwa, klabu itatozwa faini na Kamati ya Ligi ya Kitaifa na Mashindano ya FKF na pia itapoteza mechi hiyo kwa kunyang’anywa alama sita na mabao manne.”

Kulingana na mkuu wa ligi na mashindano ndani ya FKF Doreen Nabwire, walipokea barua hiyo na uamuzi utatolewa kwa wakati ufaao.

“Tulipokea barua kutoka kwa Gaspo. Pia tuliwaandikia kuhusu madhara ya kutocheza mechi hiyo na kutokana na majibu yao inaonekana tayari wameshafanya maamuzi. Tutapeleka suala hilo kwa kamati ya ligi na mashindano kwa ajili ya kujadiliwa ili kutoa uamuzi wa mwisho,” alisema Nabwire.

Haya yalijiri siku mbili baada ya ndoto yao ya kunyakua taji la KPWL kuzimwa Jumapili, baada ya sare ya 2-2 dhidi ya Wadadia Women uwanjani Mumias Sports Complex katika Kaunti ya Kakamega.

Katika mechi nyingine ya ligi Alhamisi wiki jana, Gaspo ilidondosha pointi mbili muhimu baada ya kulazimishiwa sare ya 1-1 na Ulinzi Starlets katika uwanja wa GEMS Cambridge.

Vihiga chini ya kocha Boniface Nyamunyamuh, walitangazwa kuwa mabingwa wa 2022/23 siku ya Jumapili baada ya kuwalaza Nakuru City Queens 2-1 katika Uwanja wa Maonyesho ya Kilimo (ASK) Nakuru.

Ushindi huo uliifanya Vihiga kufikisha pointi 52, nne mbele ya Gaspo.

Vihiga wataenda nyumbani na kombe na Sh1 milioni.

  • Tags

You can share this post!

MITAMBO: Mtambo unaosaidia wakulima kufunga vitita vya nyasi

KFCB yatumia wasanii kupigana na wizi wa mifugo

T L