• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
Gaspo Women wapiga abautani na kuamua kucheza dhidi ya Vihiga Queens

Gaspo Women wapiga abautani na kuamua kucheza dhidi ya Vihiga Queens

NA AREGE RUTH

GASPO Women watamenyana na mabingwa Vihiga Queens katika mechi ya raundi ya mwisho ya Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL), uwanjani Police Sacco jijini Nairobi.

Gaspo kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii wamethibitisha Ijumaa kwamba watacheza mechi hiyo licha ya kwamba mnamo Jumatano wiki hii walikuwa wametangaza kwamba wangesusia kutokana na sababu za ndani.

“Baada ya mashauriano, tumeamua kwamba tutacheza mechi dhidi ya Vihiga Queens FC mnamo Jumamosi, Mei 27, 2023. Pole zetu kwa mashabiki, wapenzi na wadau wote wa klabu ya Gaspo Women kwa usumbufu wote uliojitokeza,” imesema taarifa hiyo zaidi.

Mkuu wa mawasiliano katika Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Ken Okaka, amethibitishia Taifa Spoti kuwa Gaspo itacheza mechi hiyo.

“Ninathibitisha kwamba Gaspo walituandikia barua kusema kwamba watacheza mechi yao siku ya Jumamosi dhidi ya Vihiga Queens,” Okaka amesema.

Vihiga wako kileleni mwa jedwali wakiwa na alama 52, alama tatu mbele ya Gaspo walio katika nafasi ya pili.

Baada ya mechi hiyo, Vihiga watatawazwa rasmi kuwa mabingwa wa msimu wa 2022/23. Watatunukiwa kombe na Sh1 milioni.

Mabingwa wa zamani Thika Queens watamenyana na Zetech Sparks katika uwanja wa Police Sacco wakiwa wa pili mkiani mwa jedwali. Kangemi Ladies watapambana na Wadadia Women katika Shule ya Upili ya Dagoretti jijini Nairobi.

“Itakuwa mechi ya mapema lakini tunataka kumaliza msimu kwa kuonyesha mchezo wa kiwango cha juu. Tunatarajia mechi ngumu kwa sababu tunakabiliana na timu ngumu. Tumefanya mazoezi yetu ya mwisho Ijumaa asubuhi na wachezaji wako tayari,” amesema mtaalamu wa mbinu wa Zetech Bernard Kitolo.

Kwingineko, Kisumu All Starlets FC ambao wako chini ya mstari mwekundu watakuwa wenyeji wa Trans Nzoia Falcons FC ugani Moi jijini Kisumu.

  • Tags

You can share this post!

Mamilioni ya afisa anayelipwa mshahara wa Sh21, 000...

Kamati teule yaambiwa Mackenzie alitumia genge kuua wafuasi...

T L