NA JOHN ASHIHUNDU
GOR Mahia wametwaa ubingwa wa FKF Charity Shield baada kuilaza Kakamega Homeboyz 4-2 kupitia kwa mikwaju ya peanlti ugani Kasarani.
Mechi hiyo ilimalizika kwa sare ya 1-1 katika muda wa kawaida na ilibidi matuta hayo yapigwe ili mshindi apatikane.
Gor Mahia walianza kufunga bao katika muda wa kawaida kupitia kwa Boniface Omondi dakika ya 61 kabla ya Homeboyz kusawazisha kupitia kwa Eric Ambunya dakika 10 baadaye.
KāOgalo walianza mechi hiyo kwa mashambulizi makali na ilibidi kipa Farouk Shikalo kufanya kazi ya ziada kuokoa makombora kadhaa kutoka kwa washambuliaji wa Gor Mahia wakiongozwa na Austine Odhiambo na Lawrence Juma waliofanya mashambulizi ya mara kwa mara langoni.
Gor Mahia walipata nafasi nyingine dakika ya 32 lakini Ronny Onyango aliyeandaliwa na John Macharis alishindwa kuunganisha krosi.
Baadaye, Moses Shumma alipoteza nafasi ya wazi 56 baada ya kuandaliwa pasi na Hillary Otieno, dakika chache kabla ya kombora la Lyson Muyonga kukosea kidogo kuingia.
Alpha Onyango alipiga mpira uliomfikia Boniface Omondi ambaye aliipatia Gor Mahia bao la kwanza, lakini sherehe zao zikazimwa baada ya Ambunya kuona lango dakika ya 71.