• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 11:00 AM
Gor, Tusker na Homeboyz taabani kwa kukosa timu za wanawake

Gor, Tusker na Homeboyz taabani kwa kukosa timu za wanawake

NA JOHN ASHIHUNDU

MASHARTI magumu ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) huenda yakainyima Kenya fursa ya kuwakilishwa katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika pamoja na ya Shirikisho (CAF Confederation Cup).

CAF imesisitiza kwamba klabu zitakazofuzu kwa mashindano ya msimu ujao lazima ziwe na timu za wanawake zinazoshiriki kwenye ligi nchini mwao.

Mbali na sharti hilo, ukosefu wa viwanja ni tatizo jingine, baada ya CAF kutangaza kwamba viwanja vya Nyayo na Kasarani vinahitaji ukarabati kabla ya kukubaliwa kuandaa mechi za kimataifa, na huenda mechi kubwa kama hizo zikahamishwa nchini Tanzania au Uganda.

Wawakilishi wa Kenya katika mechi za Klabu Bingwa watajulikana siku chache zijazo kati ya Gor Mahia na Tusker baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Kenya (FKF-PL), lakini timu hizo hazina timu za wanawake.

Naye mwakilishi wa Kombe la Shirikisho atajulikana baada ya fainali ya gozi la FKF kati ya Kakamega Homeboyz na Tusker FC itakayofanyika Julai 1. Lakini Homeboyz haina timu ya wanawake.

CAF imezipa klabu husika zitimize masharti yaliyowekwa kufikia Juni 30 kabla ya kukubaliwa kushiriki katika mashindano yoyote ya shirikisho hilo la bara hili.

Barua kutoka kwa makao makuu ya CAF ilisema sharti timu hizo za wanawake ziwe zikishiriki katika ligi yoyote inayotambuliwa nchini ili klabu yao ya wanaume ikubaliwe kuwakilisha taifa barani Afrika.

Ulinzi Stars, Mathare Stars na Vihiga Bullets ndizo timu pekee zilizo na timu za wanawake ligini kwa sasa.

Kadhalika, CAF imesisitiza lazima ionyeshwe thibitisho tosha kwamba klabu husika haidaiwi pesa zozote na wachezaji wa zamani wala makocha walioondoka.

Sharti la kudaiwa tayari limeiweka Gor matatani ikikumbukwa kwamba klabu hiyo majuzi ilipigwa marufuku kutokana na deni la aliyekuwa mshambuliaji wao matata, Jules Ulimwengu, raia wa Burundi.

Vile vile klabu hiyo inakumbwa na kesi dhidi ya kiungo mshambuliaji Clifton Miheso.

Klabu pia lazima ithibitishe kwamba haidaiwi na klabu yoyote kutokana na shughuli za uhamisho. Mashirika ya soka kote barani yameshauriwa yazingatie masharti hayo magumu kabla ya kutuma majina ya timu zitakazoyawakilisha.

  • Tags

You can share this post!

Rosa Buyu: Marufuku ya muda kwa wabunge wa Azimio ni njama...

Sapoti ya Wakenya iko juu, mamake Jeff Mwathi asema akiomba...

T L