• Nairobi
  • Last Updated December 6th, 2023 9:00 PM
Guinea-Bissau nari kunyoa Super Eagles tena

Guinea-Bissau nari kunyoa Super Eagles tena

NA MASHIRIKA

GUINEA-BISSAU watapania leo Jumatatu kupokeza Nigeria kichapo cha pili mfululizo timu hizo zitakapojibwaga ugani Estadio 24 de Setembro kwa mechi ya Kundi A ya kufuzu kwa Kombe la Afrika (AFCON).

Dimba hilo la AFCON litaandaliswa nchini Ivory Coast kati ya Januari-Februari 2024.

Super Eagles ya Nigeria watakuwa na kibarua kizito cha kujinyanyua ugenini baada ya Guinea-Bissau kuwapokeza kichapo cha 1-0 katika mkondo wa kwanza jijini Abuja, Ijumaa.

Kichapo kingine kwa Nigeria kitamweka kocha Jose Paseiro katika hatari ya kupigwa kalamu.

Mreno huyo alipokezwa mikoba ya Nigeria mnamo Mei 2022 licha ya kusajili matokeo duni akinoa Venezuela, walioshinda mechi moja pekee kati ya 10 katika kipindi cha miezi 18.

Nigeria, waliotawazwa wafalme wa AFCON 2023, sasa wamepoteza mechi nne zilizopita katika mashindano yote dhidi ya Algeria, Costa Rica, Portugal na Guinea-Bissau.

Kwa upande wao, Guinea-Bissau wanaselelea kileleni mwa Kundi A kwa alama saba, moja kuliko Nigeria na tano zaidi kuliko Sierra Leone.

Ni matokeo yanayoweka hai matumaini yao ya kufuzu kwa makala ya nne mfululizo ya AFCON tangu wakose fainali za 2015 nchini Equatorial Guinea.

Kwingineko, Angola watapania kulipiza kisasi dhidi ya Ghana waliowapiga 1-0 kwao uwanjani Baba Yara, Alhamisi.

Kufikia sasa, Black Stars wa Ghana wana alama saba kutokana na mechi tatu.

Wanajivunia pengo la pointi tatu kati yao na Angola pamoja na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) kileleni mwa Kundi E.

Ushindi kwa Ghana utakuwa wao wa tatu katika mechi nne zilizopita dhidi ya Angola na utawakatia tiketi ya Ivory Coast zikisalia mechi mbili za makundi.

Niger nao watakuwa wakiwinda ushindi wa kwanza katika kampeni zao za kufuzu kwa dimba hilo la Afrika, watakapoalika Algeria katika Kundi F linalojumuisha pia Tanzania na Uganda.

Algeria wameshinda mechi zote tatu zilizopita na walikomoa Niger 2-1 ugani Nelson Mandela, Alhamisi.

Niger kwa upande wao wamepoteza mechi tatu zilizopita katika mashindano yote, ikiwemo dhidi ya Madagascar waliowafinya 1-0, kwenye mchujo wa kutafuta mshindi wa tatu wa Kombe la CHAN kwa wanasoka wanaochezea ligi za nyumbani pekee mapema mwaka huu 2023.

Kichapo cha pekee ambacho Niger wamewahi kupokeza Algeria katika historia ni cha 1-0 mnamo Mei 1981, katika mechi ya kufuzu AFCON ugani Niamey.

Algeria watajitosa leo ulingoni wakijivunia kushinda mechi nane kati ya tisa zilizopita tangu Juni 2022. Wana kiu ya kufuzu kwa makala ya tano mfululizo ya AFCON tangu wakose fainali za 2012.

  • Tags

You can share this post!

Njaa yasukuma wakazi Turkana kula tunda hatari

MKU yasifu mpango wa kuzingatia utendakazi wa kila mmoja...

T L