• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Haaland alivyoweka rekodi kwa kuibuka Mchezaji Bora na Chipukizi Bora wa Mwaka katika EPL 2022-23

Haaland alivyoweka rekodi kwa kuibuka Mchezaji Bora na Chipukizi Bora wa Mwaka katika EPL 2022-23

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Erling Haaland wa Manchester City aliweka rekodi ya kuwa sogora wa kwanza kuwahi kutawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka na Chipukizi Bora wa Mwaka katika msimu mmoja wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Mabao 36 yaliyopachikwa wavuni na nyota huyo raia wa Norway msimu huu ambao ulikamilika Jumapili yamemshuhudia akivunja rekodi ya magoli mengi zaidi kuwahi kufungwa katika msimu mmoja wa EPL.

Kwa ujumla, ametikisa nyavu za wapinzani mara 52 katika mashindano yote ya muhula huu.

“Ni fahari na heshima kubwa kwamba nimekuwa mchezaji wa kwanza kuwahi kutia kibindoni mataji yote mawili katika msimu mmoja. Nashukuru wote walionipigia kura na kila mmoja aliyechangia ufanisi huo kwa njia moja au nyingine,” akasema.

Haaland, 22, alipigiwa jumla ya kura nyingi zaidi kutoka kwa umma na jopo maalumu la EPL.

Alijiunga na Man-City mwishoni mwa msimu wa 2021-22 kwa kima cha Sh8.7 bilioni kutoka Borussia Dortmund ya Ujerumani na kusaidia waajiri wake kutawazwa wafalme wa EPL. City wametwaa taji hilo mara tatu mfululizo.

Anatarajiwa sasa kuongoza Man-City ya kocha Pep Guardiola kujitwalia mataji mawili zaidi muhula huu. Man-City watavaana na majirani zao Manchester United kwenye fainali ya Kombe la FA uwanjani Wembley mnamo Juni 3, wiki moja kabla ya kutua Istanbul nchini Uturuki kupepetana na Inter Milan kwenye fainali ya UEFA uwanjani Ataturk Olympic.

Iwapo watatia kibindoni makombe matatu muhula huu, basi Man-City watafikia rekodi ya majirani zao Man-United waliowahi kutawazwa wafalme wa EPL, UEFA na Kombe la FA katika msimu mmoja wa 1998-99.

Kufikia sasa Haaland tayari ametawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Soka (FWA) kwa upande wa wanaume.

“Nimejivunia muda wa kuridhisha sana katika msimu wangu wa kwanza kwenye soka ya EPL. Kutawazwa mabingwa wa kipute hicho wikendi iliyopita mbele ya mashabiki wetu ugani Etihad lilikuwa jambo spesheli sana kwangu,” akasema Haaland.

“Haingewezekana kabisa kujishindia tuzo hizi bila ushirikiano mkubwa kutoka kwa wanasoka wenzangu, kocha, wafanyakazi wote wengine kikosini na mashabiki ambao hutuhimiza sana uwanjani,” akaongezea.

“Sasa tuna fainali mbili zaidi zinazotusubiri. Lazima tushinde mechi hizo ili tukamilishe kampeni za msimu huu kwa matao ya juu zaidi,” akasisitiza.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

  • Tags

You can share this post!

‘Pulahia’ maisha: Akothee awakumbusha ameoleka akitaja...

Njaa kutesa Wakenya hadi 2024 – Ripoti

T L