• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:55 PM
Harambee kuzikosa Sh2.5 milioni za Ababu baada ya kutandikwa na Gabon

Harambee kuzikosa Sh2.5 milioni za Ababu baada ya kutandikwa na Gabon

Na CECIL ODONGO

Harambee Stars mnamo Alhamisi Novemba 16, 2023 ilichapwa 2-1 kwenye mechi ya kwanza ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 na Gabon kwenye uga wa Stade De Franceville katika jiji la Franceville.

Kiungo wa Red Star Belgrade Kanga Guelor alifunga bao kutokana na shuti la mbali dakika ya 86 kuwapa Panther alama zote tatu nyumbani katika mechi hiyo ya Kundi F.

Kenya ilikuwa imefunga bao la kwanza kupitia Masud Juma dakika ya 40 lakini Gabon ikasawazisha dakika ya 60 kupitia kiungo Dennis Bounga anayesakata soka ya kulipwa Marekani.

Kuelekea goli la Harambee, Amos Nondi aliachilia mpira mrefu ambao kipa Anse Ngouby ambaye alikuwa amedumu kwa dakika tano pekee uwanjani, aliondoka langoni na kukosa mpira.

Masud ambaye aliuwahi mpira huo aliujaza langoni kupitia kichwa. Ngouby alikuwa amechukua nafasi ya kipa Fotso Nouby ambaye alipata jeraha na kuondolewa uwanjani dakika ya 32.

Difensi ya Kenya iliyokuwa ikivuja ilizawidi Gabon bao la pili huku Nondi akiupiga mpira kwa kichwa nyuma nao ukaangukia Bounga ambaye alimbwaga vibaya kipa Patrick Matasi.

Japo Kenya ilicheza vyema kipindi cha kwanza, vijana wa nyumbani walisinzia kipindi cha pili na Gabon ikatumia nafasi zao kutwaa ushindi kwenye ngarambe hiyo.

Harambee Stars itaondoka Gabon saa sita Ijumaa  kuelekea Cote d’Ivoire ambako watavaana na Ushelisheli kwenye uga wa Stade Felix Houphouet-Boigny in Abidjan katika mechi nyingine ya Kundi F Jumatatu.

Gabon nao watasafiri hadi Burundi ambao ndio wapinzani wao mnamo Jumapili.

  • Tags

You can share this post!

Haiya, sikujua binti yangu ni tajiri hivi, asema mamake...

Ndoa yake ni ya machozi, yangu pia vilevile. Tunaweza...

T L