KATIKA historia yake, Kenya imeshinda mechi mbili pekee za kufuzu kwa Kombe la Dunia ugenini.
Mara ya mwisho hilo kufanyika ilikuwa mnamo Novemba 11, 2011 Harambee Stars ilipoichapa Ushelisheli 3-0 ugenini.
Kabla ya hapo, Kenya ilikuwa imechabanga Mauritius 3-1 mnamo Desemba 10, 1972 kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia.
Hii leo Stars itakuwa ikilenga kufuta rekodi hiyo mbaya itakapochuana na Ushelisheli kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Ushelisheli ni mwenyeji wa mtanange huo wa Kundi F katika uga wa Stade Felix Houphoiet-Boigny jijini Abidjan, Cote d’Ivoire.
Wanavisiwa wa Ushelisheli waliamua kupelekea mechi hiyo Cote d’Ivoire kutokana na kukosa uga ambao umeidhinishwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuandaa mechi za kimataifa.
Vijana wa kocha Engin Firat walipoteza 2-1 dhidi ya Gabon mnamo Alhamisi, huku Ushelisheli ikizamishwa 9-0 na Cote d’Ivoire mnamo Ijumaa.
Kenya, Pirates ya Ushelisheli na Gambia, ambao walipoteza 3-2 dhidi ya Burundi jijini Bujumbura, hawana alama zozote katika kundi hilo.
Cote d’Ivoire almaarufu The Elephants na Burundi zinaongoza kundi hilo zikiwa na alama tatu kila moja.
Kwa mujibu wa viwango vya FIFA, Ushelisheli ipo nambari 195, huku Stars ikiwa nambari 110 na Kenya inaonekana kuwa na nafasi bora ya kuwapiku wapinzani wao leo.
Firat tayari amesisitiza kuwa lazima waishinde leo. Kenya na Ushelisheli zimekutana mara tano na Stars imeshinda mechi zote tano.
Je, Pirates ambao wapo chini ya kocha Jean Louis, 55, watafaulu mara hii kuadhibu Stars?
Firat kwa mara nyingine atawakosa wachezaji tegemeo Joseph Okumu (Reims, Ufaransa), Eric ‘Marcelo’ Ouma (AIK, Uswidi) na Daniel Anyembe (Viborg, Denmark).
“Ni wazi kuwa nitakuwa na mabadiliko mengi kwa sababu Ayub Timbe alianguka wakati wa mazoezi na akaumia. Marcelo alifanya mazoezi kwa mara ya kwanza Jumamosi na kwa hakika sidhani kama atacheza,” akasema Firat.
“Hakutakuwa na mabadiliko mengi kwa sababu tunalenga kushambulia na kuzuia,” akaongeza.