Na MASHIRIKA
NAHODHA wa timu ya taifa ya Uingereza, Harry Kane, amejiunga Bayern Munich kwa mkataba wa miaka minne.
Nyota huyo ambaye amekatiza uhusiano wake wa muda mrefu na Tottenham Hotspur, ameyoyomea Ujerumani kwa kima cha Sh15.6 bilioni.
Kane, 30, anabanduka Spurs akiwa mfungaji bora wa kikosi hicho baada ya kupachika wavuni mabao 280 kutokana na mechi 435.
“Nahisi huu ndio wakati mwafaka zaidi wa kuondoka,” akasema Kane kupitia mtandao wake wa kijamii.
Kane alihusishwa na uwezekano mkubwa wa kujiunga na Manchester City mnamo 2021 na mustakabali wake kitaaluma ulimulikwa pakubwa muhula huu kwa kuwa alikuwa amesalia na mwaka mmoja pekee katika kandarasi yake na Spurs.
Alikuwa pia akimezewa mate na Manchester United na Real Madrid muhula huu kabla ya kufikia uamuzi wa kutua Bayern na kufanyiwa ukaguzi wa kiafya, Ijumaa.
“Tulikuwa na mazungumzo ya muda mrefu na Kane pamoja na wawakilishi wake. Lengo letu lilikuwa kurefusha mkataba wake Spurs,” akatanguliza mwenyekiti Daniel Levy.
“Hata hivyo, alisisitiza kuwa anatamani kupata changamoto mpya kwingineko. Ilibidi tumuachilie japo shingo upande,” akaongeza.
Kane ameibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mara tatu – 2015-16, 2016-17 na 2020-21. Akijivunia mabao 213 kutokana na mechi 320 katika EPL, alihitaji magoli 48 zaidi kuvunja rekodi ya nguli Alan Shearer ambaye ni mfungaji bora wa muda wote katika historia ya kipute hicho.
Kane ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Uingereza kwa mabao 58 na aliibuka pia mfungaji bora katika fainali za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi baada ya kucheka na nyavu mara sita. Hata hivyo, hajawahi kunyanyua taji lolote la haiba kubwa katika ngazi ya klabu au timu ya taifa.
“Nina furaha kubwa kuwa sehemu ya Bayern FC sasa. Hii ni mojawapo ya klabu kubwa zaidi duniani na nimesema mara kwa mara kwamba nataka kushindana ili nidhihirishe uwezo wangu katika ngazi ya juu zaidi kitaaluma,” akasema Kane ambaye atavalia jezi nambari tisa kambini mwa Bayern hadi mwaka wa 2027.
Bayern walijizolea taji lao la 33 la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) msimu jana. Ilikuwa mara yao ya 11 mfululizo kutwaa kombe hilo na wamenyanyua pia taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mara sita na German Cup mara 20.
Kane alijiunga na akademia ya Spurs mnamo 2004. Alitia saini mkataba wake wa kwanza kitaaluma mnamo 2010 na akawajibishwa katika kikosi cha kwanza mwaka wa 2011.
Bao alilofunga katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Man-City mnamo Februari 2023 lilikuwa lake la 267 kambini mwa Spurs na lilimwezesha kuvunja rekodi ya Jimmy Greaves aliyekuwa mfungaji bora wa muda wote wa kikosi hicho.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO