• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Homeboyz yalimwa winga wake David Odhiambo akitawazwa Mchezaji Bora Ligi Kuu ya Kenya mwezi Mei

Homeboyz yalimwa winga wake David Odhiambo akitawazwa Mchezaji Bora Ligi Kuu ya Kenya mwezi Mei

Na GEOFFREY ANENE

KAKAMEGA Homeboyz imeharibu siku nzuri ya winga wake David Odhiambo baada ya kupoteza 1-0 mikononi mwa Nairobi City Stars kwenye Ligi Kuu, Jumamosi.

Odhiambo alikuwa amepokea tuzo ya mwanasoka bora kwenye ligi hiyo ya klabu 17 saa chache kabla ya mchuano huo wa raundi ya 19.

Nicholas Kipkirui alifungia “Simba wa Nairobi” City Stars bao hilo la pekee dakika ya 63. Homeboyz itajilaumu yenyewe kwa sababu ilipata fursa ya kuona lango ya kwanza dakika ya 46, lakini penalti ya Christopher Masinza ikapanguliwa na kipa Steve Njunge.

Odhiambo alipata tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Mei baada ya kufungia Homeboyz mabao matatu na kumega pasi moja iliyozalisha goli.

Alianza mwezi Mei kwa kufunga bao na kusuka pasi katika ushindi wa 4-0 dhidi ya majirani wao Western Stima.

Kisha, alitikisa nyavu mara mbili katika mechi iliyofuata ambayo Homeboyz ililemea Posta Rangers 3-1 ugani Utalii.

Katika kura ya kutafuta mchezaji bora wa Mei iliyofanywa na paneli ya ligi hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya kamari ya Betking, Odhiambo alibwaga kiungo wa Sofapaka, Lawrence Juma kwa kura 5-2.

Winga wa Ulinzi Stars Clinton Omondi alikamata nafasi ya tatu.

Juma alimaliza katika nafasi ya pili baada ya kuchangia magoli mawili na pasi moja iliyozaa matunda naye Omondi alipachika mabao mawili.

Odhiambo ni mchezaji wa tano kupokea tuzo hiyo na Sh50,000 baada ya Elvis Rupia (AFC Leopards), Henry Meja (Tusker), William Wadri (Bandari) na Kelvin Opiyo (Posta Rangers) walioibuka bora mwezi Desemba, Januari, Februari na Machi, mtawalia.

You can share this post!

Mshambuliaji Memphis Depay sasa ni mali ya Barcelona

Marufuku dhidi ya Ngii yabatilishwa, sasa atawakilisha...