• Nairobi
  • Last Updated June 2nd, 2023 5:17 PM
Ingwe imani tele itafufuka timu zikijiandaa kwa ligi

Ingwe imani tele itafufuka timu zikijiandaa kwa ligi

Na CECIL ODONGO

AFC Leopards leo ina matumaini tele ya kutokomeza wimbi la matokeo duni itakapochuana na Ulinzi Stars kwenye mechi ya Ligi Kuu ugani Thika.

Mashabiki lukuki wa Ingwe wanatarajiwa kumiminika ugani humo, baada ya serikali kufungua nchi na kuondoa baadhi ya masharti makali ya kuzuia kuenea kwa janga la corona.Wakati huo huo, mechi nyingine tano za ligi hiyo, zitasakatwa Jumamosi na nyingine tatu Jumapili kwenye nyuga mbalimbali.

Kati ya mechi zitakazokuwa na ushindani mkali, ni Gor Mahia dhidi ya Sofapaka, Tusker ikivaana na Wazito na debi ya mtaa wa mabanda kati ya Mathare United na Kariobangi Sharks.KCB, ambayo ilimaliza katika nafasi ya pili msimu uliopita, ina kibarua kigumu dhidi ya washiriki wapya Police.

Mechi kati ya Ulinzi na Ingwe huwa ngumu. Hata hivyo, Ingwe imekuwa ikiwalemea wanajeshi hao kwa misimu mitatu iliyopita.Leopards tayari imezoa alama nne msimu huu kutokana na ushindi wa 1-0 dhidi ya Tusker na sare tasa dhidi ya KCB.

Ilipigwa 1-0 na Gor kwenye gozi la Mashemeji kabla ya kuzamishwa 2-1 na Bandari wiki jana.Ulinzi ya kocha Stephen Ochola haijapoteza msimu huu. Ilipiga Nzoia Sugar na Mathare 1-0 kila mmoja kabla ya sare ya 1-1 dhidi ya Bidco United wikendi iliyopita.Huku Leopards ikijivunia wachezaji wachanga na haina mshambuliaji baada ya kuondokewa na mastaa, Ulinzi ina wachezaji wengi walioisakatia msimu uliopita.

Safu ya nyuma ya Ingwe, hata hivyo, lazima ijihadhari na washambuliaji Kevin Ouma na Clinton ‘Aguero’ Omondi ambao wameonyesha mchezo mzuri msimu huu. Walifunga Mathare na Bidco United mtawalia.“Ni mechi ambayo lazima tujikaze na kurejelea ushindi baada ya kupoteza dhidi ya Gor na Bandari.

Kikosi changu kichanga kimeanza kuzoea mechi za ligi na hata dhidi ya Bandari tulionyesha mchezo ulioimarika sana,” akasema Kocha wa Leopards, Patrick Aussems.Katika mechi tano zilizopita kati ya timu hizo mbili, Leopards imeshinda mara nne huku mechi moja ikiishia sare tasa.

Mara ya mwisho Ulinzi ilipiga Ingwe ni mwaka 2018, ambapo wanajeshi hao walitamba nyumbani na ugenini 2-1.

You can share this post!

Pesa za Ruto zamgeukia

Mvutano kuhusu RBK wachukua mkondo mpya

T L