• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 5:29 PM
Inter roho juu ikirudiana na AC Milan nusu fainali ya UEFA

Inter roho juu ikirudiana na AC Milan nusu fainali ya UEFA

NA MASHIRIKA

INTER Milan watashuka ugani San Siro leo usiku wakilenga kumaliza kazi dhidi ya watani wao AC Milan na kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Masogora hao wa kocha Simone Inzaghi walitia guu moja ndani ya fainali walipoipokeza Milan kichapo cha 2-0 kwenye mkondo wa kwanza wa nusu-fainali hii, Jumatano iliyopita.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza katika miaka 18 kukutanisha miamba hao wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kwenye UEFA.

Mshindi baada ya marudiano ya leo Jumanne atakutana na Real Madrid au Manchester City katika fainali Juni 10 itakayochezewa uwanja wa Ataturk Olympic jijini Istanbul, Uturuki.

Man-City watakuwa kesho Jumatano wenyeji wa mabingwa watetezi Real ugani Etihad katika mechi ya kufa-kupona, baada ya kuambulia sare ya 1-1 katika mkondo wa kwanza ugani Bernabeu, Uhispania, Jumanne wiki jana.

Ingawa Inter wamewahi kutawazwa wafalme wa UEFA mara tatu katika historia, hawajatinga fainali tangu waibuke washindi mara ya mwisho miaka 13 iliyopita. Zaidi ya kuingia fainali ya UEFA, Inter watakuwa na kiu ya kuendeleza ubabe wao dhidi ya Milan msimu huu.

Kufikia sasa, wanakamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Serie A kwa alama 66, tano zaidi kuliko nambari tano Milan.

Baada ya kukubali kichapo cha 3-2 katika mkondo wa kwanza wa Serie A msimu huu, Inter walikomoa Milan 3-0 kwenye fainali ya Supercoppa Italiana mnamo Januari kabla kushinda mkondo wa pili wa ligi 1-0, Februari.

Licha ya kusuasua ligini msimu huu – wamepepetwa mara 11 katika mechi 35 kufikia sasa – Inter imekuwa ngangari kampeni za UEFA.

Hawajawahi kujipata nyuma katika pambano lolote la hatua ya muondoano UEFA.

Aidha, wamekamilisha mechi nne kati ya tano zilizopita UEFA bila kufungwa bao.

Iwapo Inter wataingia fainali ya UEFA basi itakuwa mara yao ya sita katika historia na ya kwanza tangu 2010.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yazuia maziwa ya Kenyatta kutoka Uganda kuingia...

Sakata ya neti za kuzuia mbu yauma wakuu wa Kemsa

T L