• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
JAGINA WA SPOTI: Huyu Sidi alikuwa kodriva ngangari katika Safari Rally

JAGINA WA SPOTI: Huyu Sidi alikuwa kodriva ngangari katika Safari Rally

NA GEOFFREY ANENE

HAITAKUWA haki kuzungumzia mashindano ya magari nchini Kenya bila kumtaja Abdul Sidi.

Sidi, 70, anafahamu kila kona ya mashindano hayo nchini kwa sababu amejishughulisha na fani hiyo ghali kwa zaidi ya miaka 40.

Alijihusisha moja kwa moja kama mwelekezi (pia dereva msaidizi) kutoka 1982 hadi 2010 alipostaafu.

Sidi alielekeza madereva maarufu Patrick Njiru, Marco Brighetti, Sammy Aslam, Bimal Shah, Phineas Kimathi, Rory Green na John Ngunjiri kutoka Kenya, Mbelgiji Gregoire de Mevius na bingwa mara nane wa Afrika Satwant Singh kutoka Zambia, miongoni mwa wengine.

Rekodi zinaonesha kuwa Sidi alianza kazi ya kuelekeza madereva mwaka 1982 akifanya shindano la Karibuni Rally akishirikiana na Asad Anwar katika gari la Datsun 160.

Hata hivyo, alichukulia majukumu hayo kwa uzito mwaka 1986 alipoelekeza Peter Hayes wakati wa Guru Nanak Rally.

Sababu ya kujitosa katika mbio za magari anasema ni dereva mkongwe Ian Duncan.

“Ilikuwa ghafla kwa sababu Duncan aliniambia niwe mwelekezi wa Peter Hayes. Nilikuwa shabiki tu wa mbio za magari kabla ya kukutana na Duncan,” akafichua Sidi aliyesoma katika darasa moja na mwanasiasa Kiraitu Murungi katika Chuka High katika kaunti ya Tharaka-Nithi.

“Nilifika kidato cha kwanza tu, lakini Mungu aliniongoza kupata maisha mazuri. Nilizuru na kushiriki mashindano barani Afrika pamoja na Malaysia,” akasema Sidi.

Kabla ya kuwa mwelekezi, Sidi alicheza soka, voliboli na mpira wa vikapu akiwa Chuka High.

Sidi anasema hakufundishwa kazi ya kuelekeza madereva na yeyote, bali mwenyewe.

Alishiriki Safari Rally mara 18 na kumaliza 15 akielekeza De Mevius, Ayub Ebrahim, Raju Limbani, Brighetti, Njiru, Aslam, Kimathi na Shusheel Shah.

Sidi alisaidia Patrick Njiru kuwa Mkenya wa kwanza mwenye asili ya Kiafrika kutawala kitengo cha Group N cha FIA Safari Rally, raundi ya WRC walipokamata nafasi ya nne kwa jumla mwaka 1994. Yanasalia kuwa matokeo mazuri kabisa kwa dereva yeyote Mwafrika kwenye WRC.

Sidi anasema kujiingiza katika mbio za magari uwe tayari kugharamika.

“Mtu hutumia zaidi ya Sh100, 000 kuweka gari lake sawa katika kila shindano. Magari haya ni ghali kuyatunza na pia kuyanunulia vifaa vipya. Kinaya ni kuwa dereva hutumia fedha nyingi kwa mashindano, lakini hakuna zawadi ya kifedha. Zawadi ni kombe na pointi tu za mashindano,” anasema.

Kufaulu kuwa mwelekezi, Sidi anashauri kuwa lazima uwe sawa kiakili na kimwili, mnyenyekevu, mwenye heshima, asiyekaribia vileo na usiwe na kiburi.

Alifichua kuwa hakuwahi kuvuta sigara, kunywa pombe, kutafuna miraa ama tumbaku. Anasema pia kuwa mwelekezi anafaa kufahamu pia dereva ni mwenye gari na mwelekezi ni abiria tu.

Akiwa mwelekezi, Sidi alisalimiana na Marais Daniel arap Moi, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta mkononi mara 16.

MATUKIO MUHIMU: Sasa ni mwalimu stadi wa mbio hizo baada ya kustaafu

Sidi aling’aa sana kama mwelekezi, sasa ni mwalimu mashuhuri wa masuala ya mashindano ya magari.

Amejihusisha na kukuza madereva na waelekezi tangu astaafu 2010; wakiwemo Helen Shiri, Tuta Mionki, Eric Bengi, Shameer Yusuf na Riyaz Ismail.

Meneja wa Usalama wa Safari Rally, Norris Ogalo, pia ni mwanafunzi wake. Ongalo ni kinara wa zaidi ya wasimamizi 500 ambao pia ni wanafunzi wa Sidi.

Baadhi ya wanafunzi wake wanaopaisha magari ama kutoa huduma za uelekezi wakati huu ni Denis Mwenda, Job Njiru, Issa Amwari, Adnan Din na Edward Njoroge.

Kuna wanafunzi kutoka Rwanda, Burundi, Tanzania na Uganda waliopitia mikononi mwake.

Itakumbukwa kuwa Sidi alihutubia kongamano la Shirikisho la Mbio za Magari Duniani (FIA), baada ya kualikwa na aliyekuwa rais wa shirikisho hilo Jean Todt nchini Rwanda mwaka 2015, lilohudhuriwa na zaidi ya mataifa 18.

Sidi amewahi kutumikia Tume ya Mbio za Magari Kenya, maandalizi ya Safari Rally 2012 na Chama cha Madereva wa mbio za magari Kenya kama mwenyekiti.

 

Marco Brighetti (kushoto) na Abdul Sidi (pili kulia) wapokea zawadi kutoka kwa waziri wa zamani Robert Ouko miaka ya hapo nyuma. PICHA | HISANI

Pia, alikuwa afisa wa habari katika Shirikisho la Mbio za Magari Kenya (KMSF), Rwanda Rally na Tanzania Rally na East African Safari Classic Rally.

Pia alikuwa mshauri wa KMSF wa masuala ya uanahabari, tasnia anayoiendeleza kwani huandika habari za mbio za magari kwenye magazeti ya kampuni ya uchapishaji magazeti ya Nation Media Group.

Isitoshe, amewahi kuwa afisa wa habari wa mashindano ya chipukizi ya Mbio za Magari Duniani yaliyodhaminiwa na Pirelli.

  • Tags

You can share this post!

Nassir apinga kulipa deni la maziwa shuleni

PENZI LA KIJANJA: Kuchagua mchumba kunahitaji hekima si...

T L