• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 7:22 PM
Jeraha la paja kumweka De Bruyne mkekani kwa miezi minne

Jeraha la paja kumweka De Bruyne mkekani kwa miezi minne

Na MASHIRIKA

KIUNGO matata raia wa Ubelgiji, Kevin de Bruyne, huenda akasalia mkekani kwa kipindi cha miezi minne ijayo huku waajiri wake Manchester City wakitarajiwa kuamua iwapo atafanyiwa upasuaji kwenye paja.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 32 aliondoka ugani akichechemea baada ya kuwajibishwa kwa dakika 23 pekee dhidi ya Burnley katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Turf Moor mnamo Agosti 11, 2023.

De Bruyne aliondolewa pia uwanjani wakati wa fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) iliyoshuhudia Man-City wakikomoa Inter Milan 1-0 jijini Istanbul, Uturuki, mnamo Juni 2023.

“Ni jeraha baya la paja. Litamweka nje kwa kipindi kirefu. Huenda akakosa tena kutuchezea kwa msimu mzima,” akasema kocha Pep Guardiola.

Kiungo huyo mzoefu alikosa kunogesha michuano yote ya kirafiki iliyosakatwa na Man-City kwa minajili ya kujifua kwa msimu huu mpya wa 2023-24. Hata hivyo, aliletwa ugani katika kipindi cha pili dhidi ya Arsenal katika kipute cha Community Shield kilichoshuhudia masogora wa Guardiola wakifungwa penalty 4-1 baada ya sare ya 1-1 ugani Wembley mnamo Agosti 6, 2023.

De Bruyne alipachika wavuni mabao 10 na kuchangia mengine 31 mnamo 2022-23 huku akisaidia Man-City kunyanyua mataji matatu – EPL, Kombe la FA na UEFA.

Man-City kwa sasa wanajiandaa kuvaana na washindi wa Europa League, Sevilla, kwenye gozi la Super Cup jijini Athens, Ugiriki, mnamo Agosti 16, 2023.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Bloga wa Jubilee Pauline Njoroge adai kuibiwa Sh300, 000...

Kuwasili kwa Moises Caicedo kwawasisimua mashabiki wa...

T L