• Nairobi
  • Last Updated June 2nd, 2023 6:24 PM
Kajiado All Stars wapepeta Kayole Youth na kutinga robo-fainali za Koth Biro Cup

Kajiado All Stars wapepeta Kayole Youth na kutinga robo-fainali za Koth Biro Cup

Na CHRIS ADUNGO

LIMBUKENI Kajiado All Stars ambao wanashiriki kipute cha Koth Biro kwa mara ya kwanza mwaka huu, wamefuzu kwa robo-fainali baada ya kuwapepeta Kayole Youth 3-2 katika mojawapo ya mechi za hatua ya 16-bora uwanjani Ziwani mnamo Jumapili ya Januari 3, 2021.

Chini ya kocha Ezekiel Akwana, Kajiado All Stars walifungua karamu ya mabao kupitia kwa Francis Githui aliyechuma nafuu kutokana na masihara ya beki Dennis Kioko wa Kayole Youth baada ya sekunde tano pekee za mwanzo wa kipindi cha kwanza.

Githui alichangia bao la pili la waajiri wake katika dakika ya 10 baada ya mpira wa kona aliouchanja kumbabatiza beki wa Kayole Youth, Dennis Kioko aliyejifunga kwa kichwa.

Ingawa Kayole Youth walianza kipindi cha pili kwa matao ya juu na kufungiwa bao na Erick Mwema katika dakika ya 55, makali yao hayakutikisa ngome ya Kajiado All Stars waliofungiwa goli la tatu na Terry Pashley Teto katika dakika ya 80.

Kioko alifungia Kayole Youth bao la pili mwishoni mwa kipindi cha pili, sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Kajiado All Stars walifuzu kwa hatua ya 16-bora baada ya kukamilisha michuano ya Kundi D kileleni kwa alama 10 mbele ya mabingwa watetezi Kingstone kutoka Shauri Moyo, Nairobi.

Licha ya idadi kubwa ya wanasoka wa Kajiado All Stars kuwa wanafunzi wa shule mbalimbali za upili katika Kaunti ya Kajiado, Akwana ni mwingi wa matumaini kwamba wavulana wake wataendeleza ubabe wao katika hatua mbili muhimu zilizosalia na hatimaye kutwaa ufalme.

“Wachezaji wangu walipata motisha zaidi baada ya kusajili ushindi katika mechi zao mbili za kwanza katika Kundi D. Haijakuwa rahisi kwa kikosi kusafiri kutoka Kaunti ya Kajiado hadi Nairobi kwa minajili ya michuano hii huku uungwaji mkono wa pekee ambao wachezaji wanapokea ukitoka kwa wazazi wao,” akatanguliza Akwana.

“Heri tupoteze kwenye fainali kuliko kubanduliwa kwenye hatua ya robo-fainali au nusu-fainali. Kutinga fainali kutatupa jukwaa zuri la kujifunza mengi kadri tunavyojiandaa kutwaa ubingwa wa makala yajayo. Hata hivyo, huenda tukaduwaza wengi na kubeba taji la mwaka huu,” akasisitiza Akwana.

Kipute cha Koth Biro ni kati ya mashindano ya zamani zaidi ya soka nchini na mapambao ya mwaka huu ni makala ya 45. Kivumbi hicho kinafadhiliwa na kampuni ya mchezo wa bahati nasibu ya Cheza Sports.

You can share this post!

Manchester City yazamisha chombo cha Chelsea na kukaribia...

Pigo kwa waandalizi wa Michezo ya Shule baada ya Rais Uhuru...