Na GEOFFREY ANENE
BINGWA wa zamani wa New York City Marathon, Geoffrey Kamworor, atatumia mbio za Great North Run mjini Newcastle nchini Uingereza kujiandaa kwa New City Marathon itakayofanyika Novemba 5 nchini Amerika.
Kamworor, ambaye alishinda New York City Marathon mwaka 2017 na 2019, atakutana na mshindi mara sita wa Great North Run Mo Farah mjini Newcastle hapo Septemba 10.
Mjini Newcastle pia kutakuwa na Muethiopia Muktar Edris, na Wahispania Hamid Ben Daoud na Daniel Mateo, miongoni mwa wengine.
Bingwa mara tatu wa Nusu-Marathon Duniani, Kamworor amethibitishwa pia kushiriki New York City Marathon ambapo atakabiliana na bingwa mtetezi Evans Chebet, Waethiopia Mosinet Geremew na Shura Kitata, Mholanzi Abdi Nageeye, Mwisraeli Maru Teferi, Mbelgiji Koen Naert na Cam Levins kutoka Canada.
Orodha ya kinadada nyota wanaoshiriki New York City Marathon ni mshikilizi wa rekodi ya dunia mbio za kilomita 42 za wanawake Brigid Kosgei na mabingwa wa zamani Peres Jepchirchir (2021) na Edna Kiplagat (2010). Pia, kuna Mary Ngugi-Cooper na Waethiopia Letesenbet Gidey, Gotytom Gebreslase na Yalemzerf Yehualaw na Mwisraeli Lonah Salpeter.