• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Kane ndiye anatoshea kwa viatu vya Messi – PSG

Kane ndiye anatoshea kwa viatu vya Messi – PSG

NA MASHIRIKA

MATUMAINI ya Harry Kane kujiunga na Bayern Munich ya Ujerumani muhula huu yamedidimia baada ya nahodha huyo wa timu ya taifa ya Uingereza kujumuishwa katika kikosi cha Tottenham Hotspur kitakachopiga mechi kadhaa za kirafiki nchini Australia na Mashariki ya Mbali.

Naye kipa mzoefu raia wa Ufaransa, Hugo Lloris, anatarajiwa sasa kuagana na Spurs baada ya kutemwa katika kikosi kitakachotegemewa na kocha Ange Postecoglou katika michuano hiyo ya kujifua kwa msimu ujao wa 2023-24.

Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy, alikutana na maafisa wa Bayern mnamo Alhamisi wiki hii kuzungumzia uwezekano wa Kane kutua ugani Allianz Arena nchini Ujerumani kwa Sh14.8 bilioni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Spurs, Lloris aliachwa nje ya kikosi kilichoelekea Australia mnamo Ijumaa ili “apate muda wa kutosha kutathmini baadhi ya ofa anazozipokea kutoka kwa klabu zinazowania maarifa yake.”

Nahodha huyo wa Spurs mwenye umri wa miaka 36 amewajibikia waajiri wake hao mara 447 tangu asajiliwe kutoka Olympique Lyon ya Ufaransa mnamo 2012.

Mwanzoni mwa wiki hii, Postecoglou alikataa kuzungumzia hali ya Lloris kambini mwa Spurs licha ya kuulizwa maswali kuhusu mustakabali wa kipa huyo aliyesaidia Ufaransa kushinda Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi.

Mbali na PSG, kikosi kingine kinachofukuzia huduma za Lloris ni Inter Milan ambao watalazimika kujaza pengo la kipa Andre Onana anayehusishwa pakubwa na Man-United.

Akisalia na mwaka mmoja pekee katika mkataba wake na Spurs, tetesi zimekuwa zikimhusisha Kane na uwezekano wa kuhamia Bayern ambao sasa wameshuhudia ofa mbili walizoweka mezani kwa ajili ya mshambuliaji huyo zikikataliwa.

Japo matamanio ya Kane ni kuvalia jezi za Manchester United, mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) hawana uwezo wa kifedha wa kumsajili. Isitoshe, Spurs hawako radhi kumuuza kwa wapinzani wao katika EPL.

Klabu nyinginezo zinazohemea huduma za Kane ni Chelsea, Paris Saint-Germain (PSG) na Real Madrid wanaosaka kizibo cha mfumaji Karim Benzema aliyejiunga na Al-Ittihad ya Saudi Arabia.

Japo Bayern ndio waliopigiwa upatu wa kujinasia huduma za Kane ambaye ni mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Spurs, miamba hao wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) bado hawajafaulu kushawishi waajiri wake kumwachilia.

PSG wanatafuta fowadi atakayejaza nafasi ya Lionel Messi, ambaye ameyoyomea Amerika kuchezea Inter Miami. PSG huenda pia wakakatiza uhusiano wao na wavamizi Neymar na Kylian Mbappe ambaye amesisitiza kuwa hatarefusha kandarasi yake ugani Parc des Princes.

Mnamo Jumatatu, Postecoglou alisema alikuwa na nia ya kumfichulia Kane mikakati na mipango kabambe aliyo nayo kuhusu jinsi ya kutambisha Spurs na kurejesha hadhi ya kikosi hicho katika soka ya Uingereza na bara Ulaya.

Aidha, alidokeza uwezekano wa Kane kupokezwa majukumu mapya katika benchi ya kiufundi ya Spurs baada ya kuangika daluga zake. Kinachosubiriwa sasa ni kuona iwapo nyota huyo atabanduka au atashawishika kusalia Spurs ambao wamemwahidi mshahara mpya wa Sh72 milioni kwa wiki kutoka kwa ule wa Sh37 milioni anaotia mfukoni kwa sasa kila baada ya siku saba.

Spurs walitua Australia mnamo Ijumaa kujiandaa kwa pambano la kirafiki dhidi ya West Ham United jijini Perth, Jumanne. Wataelekea baadaye nchini Thailand kuvaana na Leicester City mnamo Julai 23 kabla ya kutua Singapore kupimana nguvu na Lion City mnamo Julai 26.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

  • Tags

You can share this post!

AMINI USIAMINI: Utatozwa faini ya Sh40,000 ukimgusa Quokka

Sasa yametosha!

T L