Na CECIL ODONGO
TIMU ya Taifa Harambee Stars kesho Alhamisi itakuwa na mtihani mgumu itakapokabiliana na Gabon kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia mnamo 2026.
Mechi hiyo itasakatwa katika uga wa Stade De Franceville mjini Franceville, Gabon. Mtanange huo umeratibiwa kuanza saa moja jioni.
Kenya pia imeratibiwa kusakata dhidi Ushelisheli mnamo Jumatatu wiki ijayo.
Kenya, Ushelisheli na Gabon ziko katika Kundi F pamoja na vigogo wa Afrika Côte d’Ivoire, Burundi na Gambia ambazo pia ratiba zao zipo Alhamisi na Ijumaa.
Gabon ipo nambari 86 kwenye viwango vya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), Ushelisheli nambari 195 huku Kenya ikiwa nambari 110.
Kikosi cha wachezaji 24 wa Harambee Stars kiliondoka nchini saa mbili na nusu asubuhi na kutua jijini Libreville saa saba mchana kabla ya kufululiza hadi katika mji wa Franceville, takriban umbali wa kilomita 744.5.
Kabla ya timu kuondoka nchini Kenya, Waziri wa Michezo Ababu Namwamba alikuwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kuaga Stars ambapo aliahidi kuwa timu hiyo itakuwa ikipewa tunu ya Sh2.5 milioni kwa kila mechi ambayo watakuwa wakishinda kwenye Kundi F.
“Kwa kila mechi ambayo mtakuwa mnashinda, mtapata Sh2.5 milioni. Mkishinda hizi mechi mbili za kufuzu, mtapata Sh5 milioni mkirejea nchini,” akasema Namwamba.
Waziri huyo pia alifichua kuwa marupurupu yote ambayo wachezaji walikuwa wakiidai serikali kutokana na mechi za kirafiki dhidi ya Urusi, Iran na Qatar imelipwa.
Kuelekea mechi ya kesho Alhamisi, Kenya imecheza dhidi ya Gabon mara nne ikashinda mara mbili, ikapata sare moja na ikapigwa mara moja. Mnamo 2001 wakati ambapo timu hizo zilikutana mara ya kwanza, Kenya iliichapa Gabon 2-1 kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Afrika kupitia mabao yao aliyekuwa mvamizi matata Boniventure Maruti na aliyekuwa nahodha wa Harambee Stars Robert Mambo.
Wanasoka wengi wa Gabon wanacheza soka ya kulipwa nje ya nchi. Aliyekuwa mshambuliaji wa Arsenal, na Barcelona ambaye sasa anasakatia Marsaille Pierre-Emerick Aubameyang aliachwa nje ya kikosi ambacho kitasakata dhidi ya Kenya.
Kwenye mechi hiyo ya Alhamisi, mshambuliaji wa Gor Mahia Benson Omala anatarajiwa kupangwa kwenye nafasi ya mbele na mwenzake wa Al Duhail Michael Olunga.