Na GEOFFREY ANENE
KENYA Lionesses na Kenya Shujaa watakuwa mawindoni leo Septemba 16 kwa mechi muhimu nchini Afrika Kusini na Zimbabwe, mtawalia.
Wanaraga Faith Livoi na Diana Omosso kutoka klabu ya Mwamba watapata kuchezea Lionesses kwa mara ya kwanza baada ya kujumuishwa katika kikosi cha wachezaji 15 watakaoanza mechi ya kirafiki dhidi ya wenyeji Afrika Kusini.
Kocha Dennis Mwanja amejumuisha Livoi kushirikiana na Naomi Jelagat katika safu inayofahamika kama injini ya timu naye Omosso katika nafasi ya nyuma kabisa.
Rose Otieno, Knight Otwoma na Natasha Emali wako safu ya mbele naye nahodha Enid Ouma na Diana Kemunto watacheza katika safu ya kati pembeni kushoto na kulia, mtawalia, huku Phoebe Akinyi akicheza nambari nane.
Nahodha wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande, Judith Okumu atacheza katika nafasi yake ya kawaida nambari tisa akishirikiana na Ann Goretti, Grace Okulu, Prisca Nyerere na Stella Wafula katika safu ya kati. Sharon Auma na Omosso wanakamilisha nafasi tatu za mwisho.
Naomi Muhanji pia yumo mbioni kuchezea Kenya kwa mara ya kwanza baada ya kutajwa katika orodha ya wachezaji wa akiba iliyo pia na wazoefu Evelyn Kalemera na Mercy Migongo.Hesla Khisa, Michelle Akinyi, Winnie Awino, Naomi Amuguni na Esther Juma wanakamilisha orodha ya wachezaji kwenye benchi.
Lionesses ya wachezaji 15 kila upande ililemewa na Afrika Kusini 48-0 zilipokutana mara ya mwisho miezi minne iliyopita katika Kombe la Afrika nchini Madagascar.
Kenya na Afrika Kusini wanatumia mechi hiyo kujipiga msasa kabla ya kushiriki makala ya kwanza ya mashindano ya dunia ya daraja la tatu (WXV3) na daraja la pili (WXV2) mwezi ujao nchini Milki za Kiarabu na Afrika Kusini, mtawalia.
Shujaa imekabana koo na Nigeria (11.06am) ambapo imesajili ushindi wa 34-10 na inatarajiwa kukipiga dhidi ya Namibia (1.50pm) na Zambia (4.34pm) katika Kombe la Afrika ambalo linatumika kufuzu kushiriki Olimpiki jijini Paris nchini Ufaransa mwaka 2024 na pia kuingia mashindano ya kupandishwa ngazi kushiriki Raga za Dunia msimu 2024-2025.