• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Kenya waingia Kombe la Afrika la hoki bila jasho baada ya mchujo kufutiliwa mbali

Kenya waingia Kombe la Afrika la hoki bila jasho baada ya mchujo kufutiliwa mbali

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya Kenya ya mpira wa magongo ya wanaume na ile ya wanawake zimefuzu kushiriki Kombe la Afrika kutoka ukanda wa Kaskazini-Mashariki, Shirikisho la Mpira wa Magongo Kenya (KHU) limethibitisha Jumamosi.

Mwenyekiti wa KHU, Nashon Randiek aliambia Taifa Leo kuwa Kenya na Uganda zilipata tiketi mbili zilizokuwa mezani kushiriki dimba la Afrika baada ya mashindano ya Kaskazini-Mashariki kuvutia mataifa hayo mawili pekee.

“Bado hatujapokea barua rasmi kutoka kwa Shirikisho la Mpira wa magongo barani Afrika (AfHF), ingawa tarehe ya mwisho ya timu kuingia mashindano hayo ya kufuzu ilipita Kenya na Uganda zikiwa timu za pekee kuthibitisha ushiriki wao,” alisema Randiek, siku moja baada ya AfHF kutangaza kupitia mitandao yake ya kijamii kufutilia mbali mchujo huo na kupatia Kenya na Uganda tiketi hizo Februari 5, 2021.

AfHF ilisema Ijumaa kuwa iliandaa kikao chake cha kwanza, na kutokana na athari za janga la virusi vya corona “ikatoa mwelekeo mpya, matokeo ya mkutano na mabadiliko ya ratiba yake” pamoja na kupatia Kenya (wenyeji) na Uganda tiketi.

Kenya ilifaa kuandaa mchujo wa Kaskazini-Mashariki kutoka Machi 1-7 katika klabu ya michezo ya Sikh Union Nairobi kwenye barabara ya Profesa Wangari Maathai.

Randiek alisema kuwa timu za Kenya zitaendelea na mazoezi, ingawa kwa kutegemea tarehe za Kombe la Afrika, zitaongeza ama kupunguza vipindi hivyo.

“Mwenyeji wa kombe hilo pamoja na tarehe zake bado hazijajulikana. Likifanyika baadaye mwaka huu, tutapunguza kidogo mazoezi. Likisukumwa hadi 2022, tutapunguza sana vipindi vya mazoezi,” alisema afisa huyo na kuongeza kuwa Kenya ilikuwa tayari kwa mpinzani yeyote na kutokana na viwango vyake vya juu vya mchezo, ingefuzu bila kutolewa jasho.

“Kufutiliwa mbali kwa mchujo kunatupunguzia safari wakati huu wa janga la virusi vya corona,” alisema. Kenya na Uganda zinaungana na Misri na Afrika Kusini zilizoingia Kombe la Afrika kwa sababu ya kuorodheshwa katika nafasi mbili za kwanza barani Afrika katika kitengo cha wanaume. Ghana na Afrika Kusini zinakamata nafasi mbili za kwanza katika viwango bora vya wanawake barani Afrika.

Kombe la Afrika litafanyika nchini Misri ama Afrika Kusini, mataifa mawili ambayo yana uwezo wa kuliandaa ikiwemo kuwa na viwanja vya kisasa. Mabingwa wa Bara Afrika watajikatia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia 2022.

  • Tags

You can share this post!

Rotich adhihirishia Kinyamal nani mfalme wa mbio za mita 800

Inter Milan wapiga Fiorentina na kutua kileleni mwa Serie A