• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 4:47 PM
Kigogo Sergio Ramos aagana rasmi na PSG

Kigogo Sergio Ramos aagana rasmi na PSG

Na MASHIRIKA

BEKI Sergio Ramos, 37, ameagana rasmi na klabu ya Paris Saint-Germain (PSG).

Anakuwa mchezaji wa pili wa haiba kubwa kukatiza uhusiano wake na miamba hao wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) wiki hii baada ya kuondoka kwa supastaa Lionel Messi pia kuthibitishwa.

“Naiaga hatua nyingine muhimu katika safari yangu ya maisha. Kwaherini PSG,” akaandika fowadi huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uhispania kwenye mtandao wa Twitter.

Ramos anabanduka ugani Parc des Princes baada ya kusakatia PSG jumla ya mechi 57 na kuwaongoza kunyanyua mataji mawili ya Ligue 1 tangu mwaka wa 2021 alipojiunga nao kutoka Real Madrid.

“Uongozi, utaalamu na moyo wa kujitolea ni sifa zilizojidhihirisha ndani ya Ramos. Tajriba pevu anayojivunia katika ngazi na kiwango cha juu zaidi ulingoni ni jambo linalomfanya kuwa nguli wa kweli wa soka. Ilikuwa fahari kubwa kuwa naye Paris,” akasema rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi.

Ramos, ambaye pia ni mshindi wa Kombe la Dunia na mataji mawili ya Euro, ndiye mchezaji anayejivunia kusakatia Uhispania idadi kubwa zaidi ya mechi. Aliwajibikia kikosi hicho mara 180 kuanzia 2005 hadi alipostaafu 2021. Wanaomfuata ni Iker Casillas aliyetandaza mechi 167 (2000-2016) na Sergio Busquets aliyesakata michuano 143 (2009-2022).

Kati ya mataji mengi ambayo Ramos alinyanyulia Real ni matano ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Baada ya kusumbuliwa na majeraha katika msimu wake wa kwanza ugani Parc des Princes, ilitarajiwa kwamba Ramos angeshirikiana vilivyo na Messi ili kushindia PSG ufalme wa UEFA muhula huu.

Hata hivyo, kikosi hicho cha kocha Christophe Galtier kilibanduliwa katika hatua ya 16-bora kwa mara ya pili mfululizo baada ya kichapo cha jumla ya mabao 3-0 kutoka kwa Bayern Munich ya Ujerumani.

  • Tags

You can share this post!

Mshambuliaji Rafael Leao sasa kuchezea AC Milan hadi mwaka...

Azimio wala njama kuyumbisha Mswada wa Fedha na usomaji wa...

T L