• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 10:18 AM
Kipchirchir aweka rekodi mpya ya Eldoret Marathon

Kipchirchir aweka rekodi mpya ya Eldoret Marathon

Na BERNARD ROTICH

MTIMKAJI mpya Mercy Kipchumba na bingwa wa Valencia Marathon 2016, Victor Kipchirchir, walizoa Sh3.5 milioni kila mmoja baada ya kushinda Eldoret City Marathon, jana.

Kipchirchir alinyakua taji la wanaume kwa saa 2:08:54. Alifuta rekodi ya mbio hizo za Kaunti ya Uasin Gishu ya saa 2:12:38 iliyowekwa na Matthew Kisorio mwaka 2019.

Alikamilisha mbele ya wapinzani wake wa karibu Leonard Langat (2:10:40) na Emmanuel Bor (2:11:10).Kipchirchir, ambaye hufanyia mazoezi Kaptagat, alichukua uongozi baada ya kilomita ya 21 na kudumisha kasi yake hadi utepeni.

“Maandalizi yangu yalikuwa mazuri na nilikuwa katika hali nzuri. Nilifurahia mbio ndio sababu niliamua kuanza kushambulia taji mapema,” alitanguliza Kipchirchir.

Alieleza kuwa kushiriki mashindano mbalimbali ya nusu-marathon; ikiwemo Discovery Half Marathon na Sotokoto Half Marathon, kulimsaidia kupata uzoefu muhimu.“Huwa nachanganya ukimbiaji wa kilomita 21 na 42 ili kuhakikisha niko sawa kwa majukumu yajayo, na mbinu hiyo ilizaa matunda leo.

“Barabara tulizotumia pia zilikuwa nzuri, ingawa sehemu kadhaa zilizokuwa na miinuko,” aliongeza.Katika kitengo cha kinadada, Kipchumba – ambaye alikuwa katika kundi la mbele la watu watano – alidumisha kasi yake akiwa bega kwa bega na Judith Korir, kabla kuchomoka kilomita ya mwisho.

Alivuka mstari wa kukamilisha mashindano kwa saa 2:28:07 akifuatiwa kwa karibu na Judith Korir (2:28:29) naye Jackline Chelal akaridhika na nafasi ya tatu (2:29:46).

Kipchumba alifichua kunufaika katika matayarisho yake kutoka kwa mshikilizi wa rekodi ya mbio za kilomita 42 ya wanawake, Brigid Kosgei.Wote wawili wako katika kambi ya riadha ya Kapsait chini ya kocha Erick Kimaiyo.

Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya kilomita 42 ya wanaume, Eliud Kipchoge, alipongeza washiriki na waandalizi wa makala hayo ya tatu ya Eldoret City Marathon, na kutoa changamoto kwa kila mtu kufanya ukimbiaji kuwa desturi kwao.

You can share this post!

Mzozo kuhusu mpango wa kukabidhi Mumias Sugar usimamizi mpya

Hoteli iliyovamiwa na magaidi yauzwa