• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Riadha za Dunia Budapest: Kiptum na Kosgei kuongoza timu ya Kenya kwenye mbio za marathon

Riadha za Dunia Budapest: Kiptum na Kosgei kuongoza timu ya Kenya kwenye mbio za marathon

Na AYUMBA AYODI

MTIMKAJI wa pili bora kwa kasi katika historia ya mbio za kilomita 42, Kelvin Kiptum na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya marathon ya akina dada Brigid Kosgei wataongoza timu ya Kenya kwenye Riadha za Dunia jijini Budapest, Hungary mnamo Agosti 19-27.

Bingwa wa London Marathon, Kiptum, atashirikiana na mshindi mara mbili wa New York Marathon Geoffrey Kamworor aliyekamata nafasi ya nne kwenye Riadha za Dunia 2022 nchini Amerika.

Akitaja timu ya marathon ya Kenya hapo Juni 2, mkurugenzi wa mashindano wa Shirikisho la Riadha Kenya (AK) Paul Mutwii amefichua kuwa Titus Kipruto aliyemaliza Tokyo Marathon mwezi Machi katika nafasi ya nne, pia yuko kikosini.

Michael Githae aliyenyakua medali ya shaba kwenye Jumuiya ya Madola nchini Uingereza mwaka 2022 pamoja na Timothy Kiplagat aliyepata nishani ya shaba Rotterdam Marathon mwezi Aprili, wako katika orodha ya watimkaji wa akiba.

Kosgei, ambaye alivuna medali ya fedha ya Olimpiki nchini Japan mwaka 2021, bingwa wa Tokyo Marathon Rosemary Wanjiru na Sheila Chepkirui aliyekamilisha London Marathon katika nafasi ya nne mwezi Aprili, wako katika kikosi cha akina dada.

Sally Chepyego Kaptich (nambari mbili Barcelona Marathon) na Margaret Wangari (nambari mbili Jumuiya ya Madola) wako katika ya akiba.

Kiptum aliyemaliza London Marathon kwa saa 2:01:25 pamoja na wenzake watalenga kurejesha taji la dunia ambalo Kenya ilishinda mara ya mwisho kupitia kwa Geoffrey Kirui mwaka 2017.

Akina dada kutoka Kenya walipoteza taji la dunia la marathon jimboni Oregon mwaka 2022. Ruth Chepng’etich alikuwa ameshinda 2019 jijini Doha, Qatar.

Mshindi wa nishani ya shaba ya dunia mwaka 2019 Amos Kipruto na bingwa mara mbili wa Boston Marathon Evans Chebet ni baadhi ya majina makubwa yaliyopuuzwa.

Chepng’etich, ambaye hakumaliza mbio mjini Eugene, Oregon mwaka jana, Judith Jeptum aliyepata fedha katika riadha hizo na bingwa wa Olimpiki Peres Jepchirchir hawajapata namba katika kikosi cha kinadada.

Mutwii amefichua kuwa vikosi hivyo vilichaguliwa baada ya mkutano na makocha mjini Eldoret siku ya Alhamisi.

“Tulipata kikosi hiki baada ya kuzungumza na wanariadha waliokuwa tayari kuwakilisha taifa na pia watakaokuwa na nafasi wakati huo,” amesema Mutwii, akifichua kuwa baadhi ya majina mengine makubwa yaliwachwa nje kwa sababu wameshaingia mashindano mengine.

Mutwii amesema kuwa watakutana na wanariadha waliochaguliwa, pamoja na makocha wao juma lijalo kuandaa ratiba yao ya mazoezi. Amesema kuwa itakuwa vizuri waendelee na mazoezi kivyao wakati huu.

Jopo la makocha waliochagua timu ya Kenya linajumuisha Patrick Sang, Richard Metto, David Leting na kocha mkuu Julius Kirwa kwa ushauriano na makocha wa mbio za masafa marefu Joseph Cheromei na Peter Bii.

Kikosi cha wanariadha wa Kenya wa marathon:

Wanaume Kelvin Kiptum (saa 2:01:25), Geoffrey Kamworor (2:04:23), Titus Kipruto (2:04:54). Wanariadha wa akiba: Timothy Kiplagat (2:03:50), Michael Githae (2:07:28).

Wanawake: Rosemary Wanjiru (2:16:28), Sheila Chepkirui (2:17:29), Brigid Kosgei (2:14:04). Wanariadha wa akiba: Sally Chepyego Kaptich (2:20:03), Margaret Wangari (2:23:52).

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

Kero ya Ndovu: Wakazi wa Ganze wasumbuka kupata fomu za...

Kampeni ya FIFA ya kukuza soka ya wanawake nchini...

T L