• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 12:43 PM
Kisumu All Starlets kukwaana na Ulinzi Starlets kwenye nusu-fainali Kombe la FKF

Kisumu All Starlets kukwaana na Ulinzi Starlets kwenye nusu-fainali Kombe la FKF

NA TOTO AREGE

KISUMU All Starlets itamenyana na mabingwa Ulinzi Starlets katika nusu-fainali ya Kombe la Wanawake la Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kwenye uwanja wa RVIST katika Kaunti ya Nakuru leo Jumatano.

Kisumu itatarajia kupata ushindi wa kufutia machozi, baada ya kushuka daraja kutoka Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) hadi Ligi ya Daraja la Kwanza wikendi iliyopita. Walimaliza katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wakiwa na pointi 25.

Wanajeshi walijikatia tikiti ya kufuzu kwa nusu fainali baada ya kulaza timu ya Kispeed Queens (Divisheni ya Kwanza) mabao 3-0 katika uwanja wa Moi mnamo Jumapili, Mei 14, 2023.

Mshambulizi wa Ulinzi, Fasila Adhiambo ndiye mfungaji bora wa michuano hiyo akiwa na mabao sita.

Wanajeshi hao walishinda makala ya kwanza ya shindano hilo mwaka wa 2021 baada ya kuwalaza Vihiga Queens 2-0 kwenye fainali iliyosakatwa katika Uwanja wa Maonyesho ya Kilimo,  Kaunti ya Nakuru.

Kocha mkuu wa Ulinzi Joseph Mwanzia ana matumaini kuwa timu yake itafuzu kwa fainali.

“Timu ilifika Nakuru Jumatatu na tulikuwa na mazoezi ya mwisho Jumanne asubuhi. Sina majeruhi katika timu yangu na wachezaji wote wamejipanga kwa kazi kubwa inayokuja,” alisema Mwanzia.

Katika mechi nyingine katika uwanja huo, Kibera Girls Soccer (Divisheni ya Kwanza) itamenyana na Nakuru City Queens ya KWPL.

Awali katika hatua ya robo-fainali, Kibera iliifunga Kahawa Queens (Ligi ya Mkoa) mabao 7-0 kwenye uwanja wa Ruaraka na kutinga nusu-fainali.

Kwa upande mwingine, Deborah Nakhumicha na Lenah Nasimiyu walihakikisha Nakuru imeingia nusu-fainali kwa kufunga bao kila mmoja dhidi ya mabingwa wa zamani wa KWPL Thika Queens uwanjani Ruaraka Grounds jijini Nairobi mapema mwezi huu wa Mei.

Mkufunzi wa Nakuru City Queens Chrispin Wesonga anasema timu yake iko tayari kuweka historia nyumbani.

“Hii ni mara ya kwanza kwa timu yangu kutinga hatua ya nusu-fainali ya kombe hili. Tumejipanga vyema kwa dakika zote 90 na ikitokea mikwaju ya penalti pia tuko tayari kwa kazi hiyo. Tumehamasisha mashabiki kuja kuishangilia timu yetu,” alisema Wesonga.

Ratiba ya mechi

Nakuru City Queens vs Kibera Soccer Ladies (RVIST Ground, Nakuru 12:00pm)

Kisumu All Starlets vs Ulinzi Starlets (RVIST Ground, Nakuru 3:00pm)

  • Tags

You can share this post!

Atishia kuua mpangaji kwa kunyimwa ‘tunda la ndoa’

Polisi bandia anayehangaisha wakazi Nairobi

T L