• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Kotut, Wanjiru waingia mbio za Tokyo Marathon, kivumbi kutifuliwa Machi 5

Kotut, Wanjiru waingia mbio za Tokyo Marathon, kivumbi kutifuliwa Machi 5

Na GEOFFREY ANENE

WATIMKAJI CyBrian Kotut, Bernard Koech, Titus Kipruto, Rosemary Wanjiru na Joan Chelimo Melly kutoka Kenya wamethibitisha kushiriki mbio za kwanza za Marathon Kuu Duniani mjini Tokyo, Japan hapo Machi 5.

Koech ameshiriki marathon mara sita tangu 2013, ingawa nafasi nzuri amewahi kukamata inasalia kuwa nambari mbili nchini Uholanzi kwenye mashindano ya Rotterdam Marathon 2014 na Amsterdam Marathon 2021. Muda wake bora katika mbio za kilomita 42 ni saa 2:04:09 mjini Amsterdam.

Kotut pia ametimka marathon sita, lakini amepata mataji mijini Paris, Ufaransa (2016) na Firenze, Italia (2021) na Hamburg, Ujerumani (2022). Muda wake bora ni 2:04:47 kutoka Hamburg. Kipruto amekimbia kilomita 42 mara tatu akimaliza NN Marathon mjini Rotterdam katika nafasi ya nne mwaka 2021 na nambari mbili mwaka 2022. Alinyakua taji la Milano Marathon 2022 nchini Italia. Anajivunia kuwa na muda bora wa 2:04:54.

Wapinzani wao wakuu katika kitengo cha wanaume ni bingwa wa London Marathon 2021 Sisay Lemma (2:03:36) kutoka Ethiopia, nambari mbili Hamburg Marathon Stephen Kissa (2:04:48) kutoka Uganda, mshindi wa Paris Marathon 2022 Deso Gelmisa (2:04:53) kutoka Ethiopia, Mjapani Kengo Suzuki (2:04:56) aliyemaliza Tokyo Marathon 2021 katika nafasi ya nne, na Mmoroko Mohamed Reda El Aaraby (2:06:55) aliyekamilisha New York Marathon 2021 katika nafasi ya pili.

Wanjiru aliyejitosa katika mbio za kilomita 42 wakati wa Berlin Marathon 2022 alipoandikisha muda wake bora wa 2:18:00 akimaliza katika nafasi ya pili atakabiliana na bingwa wa Berlin Marathon 2019 Ashete Bekere aliyemaliza wa pili mjini Tokyo mwaka jana (2:17:58) na nambari tatu Berlin Marathon 2022 Tigist Abayechew (2:18:03) kutoka Ethiopia, mshindi wa Seoul Marathon 2022 Chelimo (2:18:04), bingwa wa Gold Coast Marathon Lindsay Flanagan (2:24:35) kutoka Amerika pamoja na washindi Mao Ichiyama (Nagoya Marathon 2020) na Mizuki Matsuda (Osaka Marathon 2021) kutoka Japan.

Mabingwa wa Tokyo Marathon 2021 Eliud Kipchoge na Brigid Kosgei hawako kwenye orodha ya washiriki watajika. Kipchoge na Kosgei wanashikilia rekodi za dunia 2:01:09 na 2:14:04 mtawalia. Pia, wanamiliki rekodi za Tokyo Marathon 2:02:40 na 2:16:02 mtawalia.

  • Tags

You can share this post!

Kipusa atimua malofa kupanga njama ya kumtongoza wakidai...

Fahamu jinsi unavyoweza kuhifadhi mazingira kwa kutumia...

T L