• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Leicester roho juu baada ya kubwaga Man-City kwenye Community Shield

Leicester roho juu baada ya kubwaga Man-City kwenye Community Shield

Na MASHIRIKA

LEICESTER City waliendeleza ubabe wao katika soka ya Uingereza kwa kunyanyua taji la Community Shield baada ya kukung’uta Manchester City 1-0 uwanjani Wembley.

Bao la pekee na la ushindi katika mchuano huo uliokutanisha mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na wafalme wa Kombe la FA, lilipachikwa wavuni na Kelechi Iheanacho – fowadi wa zamani wa Man-City aliyeangushwa na beki Nathan Ake ndani ya kijisanduku.

Gozi hilo liliwapa Man-City ambao ni washikilizi wa taji la EPL, fursa ya kumwajibisha kiungo Jack Grealish kwa mara ya kwanza tangu aagane na Aston Villa kwa Sh15.6 bilioni wiki iliyopita.

Tangu watawazwe mabingwa wa EPL mnamo 2016, Leicester wameshuhudia ufufuo mkubwa uliowazolea Kombe la FA msimu uliopita chini ya kocha Brendan Rodgers.

Watafungua kampeni zao za msimu mpya wa 2021-22 katika EPL mnamo Jumamosi dhidi ya Wolves ugani King Power huku Man-City wakiiendea Tottenham Hotspur ya kocha Nuno Espirito siku moja baadaye.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City waliwajibisha idadi kubwa ya matineja dhidi ya Leicester ikizingatiwa kwamba wanasoka wao tegemeo wakiwemo Kevin de Bruyne, Phil Foden na Raheem Sterling wangali wanauguza majeraha waliyoyapata kwenye kipute cha Euro mnamo Juni-Julai.

Man-City wangali wanahemea huduma za fowadi Harry Kane wa Spurs kwa matarajio kwamba atajaza kikamilifu pengo la Sergio Aguero aliyeyoyomea Barcelona mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

“Leicester walicheza vizuri na walistahili ushindi. Man-City ingali na safari ndefu ya kujisuka upya japo chipukizi waliowajibishwa leo waliridhisha sana,” akasema Guardiola.

Ushindi wa Leicester ulikuwa wao wa kwanza dhidi ya Man-City nje ya mashindano ya EPL tangu Februari 1968 walipowapiga miamba hao 4-3 kwenye Kombe la FA.

Isipokuwa 2019 ambapo Man-City walinogesha Community Shield baada ya kuwa mabingwa wa EPL na Kombe la FA, washindi wa Kombe la FA wametamalaki kipute cha Community Shield mara sita kati ya misimu saba iliyopita. Ni mnamo 2018 pekee ambapo wafalme wa EPL, Man-City walikung’uta Chelsea 2-0.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Messi aagana na Barcelona kwa huzuni na machozi

Haaland afungia Dortmund mabao matatu katika German Cup