• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Liverpool waajiri kocha wao wa zamani, Matt Beard

Liverpool waajiri kocha wao wa zamani, Matt Beard

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL wamemwajiri kocha wao wa zamani, Matt Beard, baada ya kukamilika kwa kampeni za Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake nchini Uingereza (WSL) msimu huu wa 2020-21.

Beard alikuwa akishikilia mikoba ya Bristol City baada ya kocha wao mkuu, Tanya Oxtoby, kupewa likizo ya uzazi. Hata hivyo, Beard alishindwa kuzuia kikosi cha Bristol City kushushwa ngazi kutoka kipute cha WSL muhula huu.

Akidhibiti mikoba ya Liverpool, Beard, 43, aliongoza kikosi hicho kutawazwa mabingwa wa WSL mnamo 2013 na 2014.

“Nafasi ilipotokea, nilihisi kwamba ni kitu ambacho nilikuwa nikitamani sana kukifanya. Nimekuwa nikifuatilia sana maendeleo ya klabu ya Liverpool tangu niondoke. Unapokuwa nje ya klabu, ndipo unapotambua jinsi kikosi ulichowahi kukinoa kilivyo spesheli zaidi,” akasema Beard.

Liverpool hawajakuwa na kocha tangu waagane rasmi na mkufunzi Vicky Jepson mnamo Januari 2021.

Baada ya kuondoka Liverpool na kutua kambini mwa Boston nchini Amerika mnamo 2015, Beard aliajiriwa na kikosi cha West Ham United mnamo 2018.

Aliongoza kikosi hicho kutinga fainali ya Kombe la FA mnamo 2019 kabla ya kuagana nacho mwishoni mwa mwaka wa 2020 baada ya kuongoza waajiri wake hao kusajili ushindi mara moja pekee kutokana na mechi saba.

Baada ya kuaminiwa fursa ya kushikilia mikoba ya Bristol City mnamo Januari 2021 kikosi hicho kikihitaji alama nne zaidi ili kujitoa mkiani mwa WSL, Beard aliongoza klabu hiyo kushinda mechi mbili kati ya tano. Hata hivyo, Bristol City walishindwa kushinda mchuano wowote kati ya saba za mwisho wa msimu huu na hatimaye kuteremshwa ngazi hadi Ligi ya Daraja la Kwanza baada ya kujivunia misimu minne kwenye WSL.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Sheffield United kumwajiri kocha Slavisa Jokanovic wa klabu...

Commander Okoth atinga nusu-fainali ya ndondi za Urusi