Na GEOFFREY ANENE
MABINGWA wa Ligi ya Uropa 1972-1973, 1975-1976 na 2001-2001, Liverpool wametiwa katika kundi rahisi la makala ya msimu huu wa 2023-2024 huku wakipigiwa upatu kwamba watatia fora.
Vijana wa kocha Jurgen Klopp watapepetana na LASK (Austria), Union SG (Ubelgiji) na Toulouse (Ufaransa) katika Kundi E.
Mechi za makundi zitafanyika Septemba 21, 2023 hadi Mei 22, 2024.
Wafalme hao wa zamani wa Klabu Bingwa Ulaya wanaojivunia wachezaji matata wakiwemo Mohamed Salah, Darwin Nunez na Virgil van Dijk, walijipata katika mashindano hayo ya daraja ya pili baada ya kumaliza Ligi Kuu msimu jana nje ya nne-bora.
Liverpool si pekee kutoka Uingereza walipata kufahamua makundi yao.
Hata hivyo, West Ham ya kocha David Moyes na Brighton inayotiwa makali na Roberto De Zerbi, zimejipata katika makundi magumu.
West Ham, ambayo imeanza Ligi Kuu ya Uingereza vyema msimu huu baada ya kuponea tundu la sindano kushushwa ngazi msimu 2022-2023, italimana na Olympiacos (Ugiriki), Freiburg (Ujerumani) na Backa Topola (Serbia) katika Kundi A.
Itapata mtihani mkali, hasa kutoka kwa miamba wa Ugiriki, Olympiacos na Wajerumani Freiburg kwenye raundi hiyo ya timu 32.
Brighton wanaorejea katika mashindano ya Ulaya baada ya miaka 122, watapimwa vilivyo uwezo wao na miamba Ajax (Uholanzi) na Marseille (Ufaransa) katika Kundi B lililo pia na AEK Athens.
Droo ya Ligi ya Uropa (2023-2024):
Kundi A – West Ham (Uingereza), Olympiacos (Ugiriki), Freiburg (Ujerumani), Backa Topola (Serbia);
Kundi B – Ajax (Uholanzi), Marseille (Ufaransa), Brighton (Uingereza), AEK Athens (Ugiriki);
Kundi C – Rangers (Scotland), Real Betis (Uhispania), Sparta Prague (Czech), Aris Limassol (Cyprus);
Kundi D – Atalanta (Italia), Sporting (Ureno), Sturm Graz (Austria), Rakow (Poland);
Kundi E – Liverpool (Uingereza), LASK (Austria), Union SG (Ubelgiji), Toulouse (Ufaransa);
Kundi F – Villarreal (Uhispania), Rennes (Ufaransa), Maccabi Haifa (Israel), Panathinaikos (Ugiriki);
Kundi G – Roma (Italia), Slavia Prague (Czech), Sheriff Tiraspol (Moldova), Servette (Uswisi);
Kundi H – Leverkusen (Ujerumani), Qarabag (Azaerbaijan), Molde (Norway), Hacken (Uswidi).