• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:47 AM
Man-City pazuri kutinga fainali ya UEFA baada ya kulazimishia Real sare

Man-City pazuri kutinga fainali ya UEFA baada ya kulazimishia Real sare

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walijiweka pazuri kufuzu kwa fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu wa 2022-23 jijini Istanbul, Uturuki, baada ya kulazimishia Real Madrid sare ya 1-1 katika mkondo wa kwanza ugani Bernabeu, Uhispania.

Matokeo hayo yanaacha Man-City wanaofukuzia mataji matatu msimu huu katika ulazima wa kushinda Real wakati wa marudiano ugani Etihad mnamo Mei 17 ili kuweka hai matumaini ya kujizolea kombe la UEFA kwa mara ya kwanza katika historia.

Mshindi kati yao na Real atakutana ama na Inter Milan au AC Milan kwenye fainali. Inter walikomoa Milan 2-0 katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ugani San Siro, Jumatano.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City walitamalaki kipindi cha kwanza cha mchuano huo huku kipa Thibaut Courtois akiwajibishwa vilivyo na Kevin de Bruyne, Rodri na Erling Haaland.

Hata hivyo, Vinicius Jr aliwaweka Real kifua mbele katika dakika ya 36 baada ya kushirikiana vilivyo na Camavinga Eduardo kabla ya Man-City kusawazisha mambo kupitia kwa De Bruyne kunako dakika ya 67.

Man-City sasa hawajapigwa katika mechi 21 za mashindano yote na wameshinda michuano 17 kati ya hiyo. Sasa wanahitaji kushinda mechi zote saba walizosalia nazo msimu huu ili kuweka kunyanyua mataji matatu –  Kombe la FA, Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na UEFA.

Licha ya kuwa miongoni mwa vikosi bora zaidi katika soka ya bara Ulaya kwa sasa, Man-City hawajawahi kutwaa ubingwa wa UEFA.

Real walitinga hatua ya nne-bora kwenye UEFA msimu huu baada ya kudengua Chelsea kwa mabao 4-0 katika robo-fainali huku kocha Pep Guardiola akiongoza masogora wake kubandua Bayern Munich kwa jumla ya magoli 4-1.

Tofauti na Man-City wanaofukuzia mataji matatu msimu huu, Real wana muda wote wa kumakinikia marudiano ya UEFA na kutwaa taji kwa mara ya 15 katika historia baada ya Barcelona kuwapiga kumbo kwenye kampeni za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Kinachowaaminisha zaidi Real ni rekodi nzuri ya kutofuzu kwa fainali mara moja pekee katika misimu mitano iliyopita ambapo wametinga hatua ya nne-bora kwenye UEFA. Mara ya pekee ambapo Real walikosa kuingia fainali ya UEFA baada ya kufuzu kwa nusu-fainali ni 2020-21.

Chelsea, walioibuka mabingwa msimu huo, walidengua Real kwa jumla ya mabao 3-1 baada ya kupiga sare ya 1-1 katika mkondo wa kwanza jijini Madrid, Uhispania, na kusajili ushindi wa 2-0 wakati wa marudiano ugani jijini London, Uingereza.

Real walijibwaga ulingoni kwa mkondo wa kwanza dhidi ya Man-City wakijivunia kushinda mechi tano mfululizo za UEFA huku wakiwa wamekamilisha michuano mitatu ya awali katika kipute hicho bila kufungwa bao.

Sasa wamepachika wavuni magoli 17 katika UEFA tangu Paris Saint-Germain (PSG) iwafunge 1-0 katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora nchini Ufaransa mnamo Februari 15, 2022.

Hata hivyo, miamba hao hawajakamilisha mechi tano zilizopita katika mashindano yote bila kufungwa bao. Kusuasua huko kunatazamiwa kuchochea motisha ya Man-City wanaopigiwa upatu wa kuchuma nafuu kutokana na wingi wa mashabiki wao wa nyumbani ugani Etihad.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Maajabu mashemeji wakicharaza baba ya mume

DPP aomba aliyetapeli wabunge nusu milioni asalie gerezani

T L